KHARTOUM : Waasi waachilia mateka 36 wa Umoja wa Afrika
10 Oktoba 2005Kikundi kilichojitenga cha waasi wa Dafur kimewaachilia huru mateka 36 wa Umoja wa Afrika lakini bado kinaendelea kuwashikilia mateka wengine wawili katika jimbo hilo la magharibi mwa Sudan.
Umoja wa Afrika AU umekilaumu kikundi hicho kilichojitenga na waasi wa JEM kwa kuhusika na utekaji nyara huo hata hivyo kikundi hicho kimekanusha shutuma hizo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Afrika kikundi hicho kwanza kiliteka timu ya wanajeshi wa nchi mbali mbali wa Umoja wa Afrika yenye kusimamia usitishaji wa mapigano hapo Jumapili na baadae ikaishika timu ya uokozi katika mji wa Tine ulioko kwenye mpaka kati ya Chad na Sudan.
Msemaji wa Umoja wa Afrika Noureddine Mezini amesema mkuu wa kikosi cha Umoja wa Afrika ameshuhudia kuachiliwa kwa mateka hao 36.
Amesema 26 wameachiliwa na wawili ambao bado wanaendelea kushikiliwa na kundi hilo ni mkuu wa timu ya Umoja wa Afrika na mkalimani.
Duru za Umoja wa Afrika zilizokataa kutajwa jina zinasema kundi hilo la waasi lililojitenga na uongozi wa kundi la JEM mapema mwaka huu lilikuwa likidai kupatiwa nafasi katika mazungumzo ya amani kwenye mji mkuu wa Nigeria Abuja.