KHARTOUM:Wanajeshi zaidi ya 10 wa Umoja wa Afrika wauwawa Darfur
30 Septemba 2007Wanajeshi zaidi ya 10 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Sudan wameuwawa katika shambulio lililolenga kambi yao kwenye eneo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo. Wanajeshi wengine 7 wamejeruhiwa .Shambulio hilo ndilo baya kabisa kuwahi kushuhudiwa na kikosi hicho tangu kitumwe jimboni Darfur mwaka 2004. Wanajeshi wa Sudan na makundi ya waasi wanalauminiana juu ya shambulio hilo liliofanyika jumamosi usiku katika kambi ya Hakskanita.
Msemaji wa jeshi la Umoja wa Afrika amesema kiasi cha wanajeshi 40 wametoweka tangu jana usiku ingawa idadi hiyo haijathibitishwa.Kamanda wa Kundi la waasi la JEM katika eneo hilo Abdel Aziz el Nur Ashr amesema vikosi vyake viliondoka Haskanita siku nne zilizopita ili kutoa nafasi kwa opresheni nyingine na ameilaumu serikali juu ya shambulio hilo. Hivi karibuni rais Omar Hassan el Bashir alisema atazingatia makubaliano ya amani wakati mazungumzo yatakapoanza lakini kiongozi wa kundi la haki na Usawa JEM Khalil Ibrahim alisema hatakomesha mapigano hadi makubaliano ya amani yafikiwe.Mazungumzo yamepangwa kufanyika mwezi ujao nchini Libya.