1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Kherson washangiria kuondoka wanajeshi wa Urusi

13 Novemba 2022

Mamia ya wakaazi wa mji wa Kherson wamejitokeza mitaani kuwakaribisha wanajeshi wa Ukraine baada ya wanajeshi wa Urusi kujiondowa katika kile kinachotafsiriwa kuwa ni pigo kubwa kwa kampeni ya kijeshi ya Moscow.

Ukraine Kiew | Menschen feier die Rückeroberung Cherson
Picha: GENYA SAVILOV/AFP

"Sote tumekomboka", alisema Rais Volodymyr Zelensky siku ya Jumamosi (Novemba 12) baada ya kutangaza siku moja kabla kwamba mji huo wa Bahari Nyeusi ulikuwa mikononi mwa Kyiv.

Mji wa Kherson ulikuwa wa kwanza mkubwa kuingia mikononi mwa Urusi baada ya uvamizi wa mwezi Februari.

"Kabla ya kukimbia Kherson, wavamizi waliharibu miundombinu yote - mawasiliano, maji, umeme na gesi," alisema Zelensky, akiongeza kwamba takribani mabomu 2,000 yameteguliwa.

Alisema vikosi vya Ukraine vimetwaa udhibiti wa maeneo zaidi ya 60 katika mkoa wa Kherson.

Baada ya miezi minane ya ukaliaji wa Urusi, televisheni ya Ukraine imerejesha matangazo yake kwenye mji huo na shirika la nishati la mkoa huo linaendelea na kazi ya kurejesha huduma ya umeme.

Mkuu wa polisi ya Ukraine, Igor Kylmenko alisema kiasi cha maafisa 200 wameweka vizuizi vya barabarani na kuanza kusajili uhalifu uliotendwa na wavamizi wa Kirusi.

Ngome pekee ya Urusi ndani ya Ukraine

Wanajeshi wa Ukraine wakiingia Kherson.Picha: Ashley Chan/Zuma/picture alliance

Kherson ulikuwa moja kati ya mikoa minne ya Ukraine ambayo Rais Vladimir Putin alidai kuiunganisha na nchi yake mwezi Septemba.

Lakini wiki kadhaa baadaye,kujiondowa kwa wanajeshiwake kwenye mji mkuu wa mkoa huo, unaoitwa pia Kherson, kumeimarisha hamasa ya wanajeshi na wananchi wa Ukraine baada ya miezi tisa ya mapambano na hali ngumu ya maisha.

Katika kijiji kilichokuwa kikikaliwa na wanajeshi wa Urusi, Pravdyne, nje kidogo ya Kherson, wananchi wanaorejea kwenye makaazi wao waliwakumbatia majirani, huku wengine wakishindwa kuyazuwia machozi yao. 

"Hatimaye ushindi umepatikana!" Alisema Svitlana Galak, ambaye amempoteza bintiye mkubwa kwenye vita hivi. 

"Tunamshukuru Mungu tumekombolewa na kila jambo sasa litakuwa sawa," mwanamke huyo wa miaka 43 aliliambia shirika la habari la AFP, huku mumewe, Viktor mwenye umri wa miaka 44, akiongeza: "Sisi ni Ukraine."

Mabomu yateguliwa

Baadhi ya magari ya kijeshi ya Urusi yaliyotelekezwa na kuteketezwa katika mkoa wa Kherson.Picha: Celestino Arce Lavin/ZUMA/IMAGO/ZUMA Wire

Vifaru na mabomu kadhaa yaliweza kuonekana kwenye makaazi ya watu lilipo pia Kanisa Katoliki la Poland na majengo mengine yaliyoharibiwa.

Akizungumza kutoka katikati ya mji wa Kherson, mkuu wa utawala wa mkoa huo, Yaroslav Yanushevych, alisema kila kitu "kilikuwa kinafanywa ili kuyarejesha maisha kwenye hali ya kawaida" kwenye eneo hilo.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuteguwa mabomu ya ardhini, na kwa hilo serikali ya mkoa huo imelazimika kutangaza amri ya kutotoka nje, alisema Yanushevych katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na inayoonesha mamia ya watu wakishangiria mitaani.

Picha zilizosambazwa na jeshi la Ukraine zinaonesha wakaazi wa Kherson wakicheza huku wakiimba wimbo wa kizalendo uitwao "Chervona Kalyna".