Kiapo cha rais Putin kuongoza Urusi
8 Mei 2018Katika uhariri wake Kolner Stadt-Anzeiger linalotoka mjini Cologne limeandika juu ya kile anachojivunia Putin wakati akiingia muhula wa nne wa utawala wake. Linaandika kuwa Putin anasherehekea miujiza mipya ya silaha na mashujaa wake wa vita. Lakini ilionekana kama kwamba anajivunia pia maajabu ya kiuchumi ambayo katika hali halisi hayapo. Pato limebakia kama lilivyo kwa miaka mingi sasa, wenye maarifa wanakimbilia nchi za nje, ukandamizaji wa wapinzani wake limekuwa takriban jambo la kila siku. Pamoja na yote hayo, Putin anazidi kung'ara, akitoa sura ya kwamba Urusi inakwenda sambamba na yale yaliokuweko enzi za muungano wa Kisovieti."
Gazeti la Badische Zeitung linalotoka mjini Freiburg, nalo limejikita katika mada hiyo ya muhula wa nne wa rais Putin na haja ya kujenga hali ya kuaminiana kati ya Urusi na nchi za magharibi. Gazeti hilo linaandika kuwa Kile kilichowazi ni kwamba Urusi na upande wa magharibi zimeingia katika hatua ya Putin na muhula wake wa nne. Putin anaendelea kuwa Rais na kutokana na hayo yeye na wenzake wa magharibi, watakuwa na kazi ya kujenga hali ya kuaminiana, jambo ambalo Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alilipigania lakini kikweli hakujaribu kulifikia na ambalo ni muhimu katika kuleta wizani na kupigania kwa dhati hali ya kuaminiana kati ya Mashariki na Magharibi.
Frankfurter Allgemeine Zeitung, linaandika kuwa , hotuba ya Putin hapo jana Jumatatu baada ya kuapishwa ,ilielekea upande tafauti kabisa. Linasema Vladimir Putin aligusia maswala kadhaa. Lakini kukithiri kwa rushwa ni utaratibu wa utawala wake, kutofanya kazi barabara kwa sheria panapohusika na wajasiriamali wadogo na wa tabaka la kati ni matukio ya kila siku yakiandamwa na urasimu mkubwa.
Kuhakikisha ushindi wake, kulitegemea sera zake za ndani, jambo ambalo pia lilizingatia uhusiano wa Putin na ulimwengu uliosalia. Anapozungumzia amani, majadiliano na ushirikiano katika hali ya usawa, kuna watakaopongeza ,kwa kusema kuwa Urusi kuna demokrasia, wakati sivyo hata kidogo Na hapo ndipo inaposhangaza kumuona Kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröder akiwa mstari wa mbele kwenye sherehe ya kuapishwa mtawala huyu, Vladimir Putin.
Gazeti la Die Welt linalotoka mjini Berlin , lilijikita pia na kuwepo kwa Kansela wa zamani wa Ujerumani Schöder katika hafla ya jana ya kuapishwa rafiki yake Putin. Katika hali ya kutofurahishwa na kuhudhuria kwake, gazeti hilo limeandika kwamba Inasumbua mno kumuona Kansela wa zamani wa Ujerumani akiwa katika hafla hiyo. Na muhimu nyuma ya Schröder alikuwa ni mcheza sinema Steven Seagal ambaye mafanikio yake ya mwisho yalikuwa ni miaka 20 iliopita. Kila unapoendelea kuiangalia picha ile ya kufedhehesha ndipo inapokuwa wazi kwamba hapa ndipo Schöder alipofikia. Ni Steven Seagal wa siasa za kimataifa.
Mwandishi : Mohammed Abdul-Rahman/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu