1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miongoni mwa waliofariki ni madaktari 2 wa WHO na dereva

11 Aprili 2019

Umoja wa mataifa umesema kiasi cha watu 56 wameuliwa huku 266 wakijeruhiwa katika muda wa siku sita nchini Libya ambako vikosi vya jeshi la Mashariki mwa Libya vinakabiliana na vikosi vitiifu kwa serikali ya Tripoli

Libyen Mitglieder der National Army LNA in Bengasi
Picha: Reuters/E. O. Al-Fetori

Taarifa hiyo ya umoja wa mataifa haikufafanua wengine waliofariki ni raia wa kawaida ama ni wanajeshi wanaoshiriki makabiliano hayo ambapo mbabe wa kijeshi anayeongoza eneo la Mashariki mwa Libya Khalifa Haftar wiki iliyopita aliamrisha jeshi lake kwenda kuuteka mji wa Tripoli.

Jeshi hilo la taifa la Libya linaloongozwa na Haftar (LNA) hadi leo asubuhi lilikuwa limeshikilia vitongoji mbali mbali kilomita 11 kusini mwa mji mkuu Tripoli ambako vita vinaendelea na hadi sasa maelfu wamekimbia makaazi yao.

Mwanachama wa kamati ya mizozo katika manispaa ya Tripoli, Nasser Al Kario  aliliambia shirika la habari la Ujerumani (DPA) kwamba janga la binada mu linaweza kufika katika mji mkuu iwapo vita hivyo vitaendelea na kuingia ndani ya mji wa Tripoli ambapo kuna watu  zaidi ya milioni mbili.

Mbabe wa kijeshi anayeongoza eneo la Mashariki mwa Libya Khalifa Haftar Picha: picture-alliance/ Balkis Press

Al Kario alisema kamati yake haina rasilimali za kutosha kushughulikia ongezeko lisilotarajiwa la raia wasio na makaazi na iwapo vita hivyo havitositishwa basi wanatarajia maelfu ya watu kuachwa bila makao.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataida Antonio Guterres alitaka vita hivyo kusitishwa ili kuepuka umwagikaji mkubwa wa damu mjini Tripoli huku akiwaambia wanahabari kwamba kuna wasiwasi mkuu sio tu kwa maisha ya watu wa Libya bali pia kwa wahamiaji na wakimbizi mjini Tripoli na raia wa kigeni na kwa hivyo wana kila sababu ya kutaka vita hivyo kusistishwa.

"Ni wakati wa kusitisha vita. uko muda wa kuweka chini silaha, ili kukomesha vita kuendelea na kuepuka maafa zaidi ambayo yatakuwa ni vita vya damu kumwagika. Ninafurahi shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi liliweza kuhamisha moja ya kambi ya wakimbizi. Ni wazi kabisa kwangu kwamba tunahitajika kuanza upya mazungumzo ya dhati ya kisiasa ila bila shaka hayo hayawezi kufanyika bila kusimamisha vita hivi kabisa," alisema Guterres.

Mwito wa amani washinikizwa

Spika wa bunge la Libya upande wa Mashariki Aguila Saleh ameliambia shirika la habari la Associated Press nchini Misri kwamba hawawezi kufanya makubaliano ya amani kwa sasa baina ya pande hizo mbili hasimu kwa sababu mji mkuu wa Tripoli umetekwa na makundi yaliyo na silaha na kwamba jeshi la Haftar limeingia kuikomboa Tripoli.

Gari la jeshi la serikali ya Tripoli Picha: Reuters/I. Zitouny

Balozi wa Umoja wa Mataifa nchini Ujerumani Christoph Heusgen ambaye ni kiongozi wa baraza la usalama kwa sasa amesema wanachama wake pia wametaka silaha kuwekwa chini na kuhimiza mazungumzo na kupata suluhu ya kisiasa.

Taifa la Libya lilitumbukia katika machafuko baada ya majesho ya muungano wa NATO kuunga mkono vuguvugu la kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo marehemu Muammar Gaddafi ambaye baadaye aliuliwa mwaka 2011. Uchaguzi ulifanyika punde baada ya kuuwawa Gaddafi ila haikuweza kuleta ustawi wa taifa hilo hadi sasa.

Nchi hiyo iliyo na utajiri wa mafuta Kazkazini mwa bara Afrika hivi sasa inasimamiwa na tawala zinazohasimiana, ambazo ni serikali inayoungwa mkno na Umoja wa Mataifa iliyoko mjini Tirpoli na eneo la Mashariki linaloongozwa na Khalifa Haftar.

(RTRE/DPAE/APE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW