Kiasi watu 350,000 wamehamishwa kutokana na mafuriko
26 Agosti 2010Mto Indus katika eneo la kusini ya jimbo la Sindh nchini Pakistan umezamisha vijiji vingine kadha leo , na maafisa wameamuru watu zaidi ya 350,000 kuhamishwa.
Kiasi cha watu laki tatu hadi laki tatu na nusu wataathirika katika eneo la Thatta, ambalo ni wilaya inayoishi karibu watu laki nane, amesema Kher Mohammad Kaloro, mkurugenzi wa mamlaka ya operesheni za uokozi katika jimbo lililokumbwa na maafa la Sindh.
Mafuriko yamevunja matuta mamwili, ya kuzuwia maji na kuilazimu serikali kuwaomba watu kuondoka kutoka katika eneo hilo la Sajawal, mtu mdogo unaoishi watu wapatao 28,000. Maji pia yanaelekea katika miji ya Qambar na Shadadkor na watu wengi zaidi wataathirika ameongeza Kaloro.
Mara baada ya tangazo hilo kutolewa kwa njia ya vipaza sauti katika misikiti mjini Sajawal, biashara zilifungwa na watu walianza kufunga chochote walichonacho ambacho wanaweza kukichukua.
Mamia ya watu wamekimbia mji huo kwa magari, malori na mikokoteni ya ng'ombe. Jeshi hata hivyo lilikuwapo kuwaokoa watu ambao huenda wakaachwa . Meja jenerali Shaukat Iqbal , kamanda wa jeshi katika eneo hilo, amesema kuwa maboti ya jeshi la majini yatatumika na helikopta mbili zinaangalia hatua hizo za uokozi.
Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa za masika mwezi mmoja uliopita yameathiri zaidi ya watu milioni 17.2, ikiwa ni pamoja na watu milioni 3.8 katika jimbo la Sindh, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,500 kwa mujibu wa mamlaka ya kushughulikia maafa nchini Pakistan.
Daniele Donati wa shirika la kilimo na chakula la umoja wa mataifa FAO amesema kuwa hekta milioni 3.2 za mazao zimeharibiwa na mafuriko na kwamba ng'ombe wapatao 200,000 wameuwawa katika jimbo la Sindh na Khyber-Pakhtunkhwa pekee.
Wafanyakazi wa kutoa misaada wamekuwa wakihangaika kuwafikia watu waliotawanyika ambao wanaishi hivi sasa katika kambi za kutolea misaada, ama wako katika maeneo ya wazi wakiwa hawana chakula , dawa ama maji safi ya kunywa.
Umoja wa mataifa umesema wiki hii kuwa kiasi watu 800,000 bado wamekwama ambapo hawana mawasiliano na sehemu nyingine za nchi hiyo, na zinahitajika helipokta zaidi kuwapelekea vyakula.
Waziri wa kilimo cha umwagiliaji katika jimbo la Sindh amesema kuwa maji yamekuwa yakileta mbinyo dhidi ya matuta ya kuzuwia maji katika vijiji vya Garni Khuda Bakhsh, ambako waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhuto na baba yake, pamoja na kaka zake wawili wamezikwa.
Katika eneo karibu na bahari ya Arabia , maafisa wanahofu kuwa wilaya ziliziko katika maeneo ya pwani huenda zikakumbwa na mafuriko katika siku zijazo, kutokana na mafuriko kusogea upande wa kusini pamoja na dhoruba baharini.
Katika harakati za uokozi , shirika la kimataifa la wahamiaji IOM limesema kuwa watu milioni 4.5 bado wanahitaji sehemu za kuishi kwa dharura.Mjini Washington ambako serikali ya Marekani imeiweka Pakistan katika mstari wa mbele katika juhudi za kupambana na kundi la Taliban nchini Afghanistan , afisa wa Marekani amesema kuwa Taliban wanapanga kuwashambulia wafanyakazi wa kigeni wa kutoa misaada ambao wako katika kazi ya kusambaza misaada.
Mwandishi: Sekione Kitojo / AFPE / DPAE
Mhariri: