Kiasi watu sita wauwawa katika shambulio mjini London
4 Juni 2017Washambuliaji watatu, ambao walikuwa wamevalia mikanda ya bandia ya miripuko , pia walipigwa risasi na polisi na wamefariki, polisi ya mjini London imesema.
"Katika wakati huu, tunaamini kwamba watu sita wameuwawa pamoja na washambuliaji watatu waliopigwa risasi na polisi," amesema kamishna msaidizi Mark Rowley , ambae pia ni mkuu wa kitengo cha kupambana na ugaidi.
Washukiwa waliwagonga wapita njia katika daraja la London kabla ya kuwashambulia watu katika baa za karibu na migahawa, Rowley alisema. Polisi wenye silaha waliwapiga risasi washambuliaji watatu katika muda wa dakika nane baada ya polisi kupokea siku ya kwanza ya kuhusiana na mashambulio hayo ya kigaidi katikati ya London usiku wa Jumamosi, amesema.
Simu ya kwanza ilipokelewa baada ya washambuliaji kuendesha gari yao na kuwagonga wapita njia katika daraja la London kabla ya kuwachoma visu watu katika soko la karibu la Borough, Rowley amesema.
Watu walioshuhudia waliliambia gazeti la Guardian waliwaona watu wawili wakiwachoma visu watu nje ya mgahawa maarufu wa Roast katika soko la Borough. "Niliwaona watu wawili wakiwa na visu vikubwa nje ya mgahawa huo wa Roast," mpishi kutoka katika mgahawa wa karibu aliliambia gazeti hilo.
Polisi wachukua hatua ya haraka
Walikuwa wakiwachoma visu watu , tulikuwa tunapiga kelele "acha, acha" na watu walikuwa wakiwatupia viti," mpishi huyo alisema. "polisi walikuja na kuwapiga risasi watu hao moja kwa moja."
Waziri mkuu Theresa May aliliita shambulio hilo kuwa "tukio la kigaidi" na alieleza "shukrani zake nyingi" kwa polisi na huduma za dharura. Meya wa London Sadiq Khan amesema anapanga kuhudhuria mkutano mapema leo Jumapili (04.06.2017) wa kamati ya dharura ya serikali inayojulikana kama cobra, ambayo inatarajiwa kuongozwa na waziri mkuu May.
"Mpaka sasa hatufahamu maelezo zaidi, lakini hili lilikuwa shambulio la makusudi na la waoga dhidi ya wakaazi wa London ambao hawana hatia na watu wanaotembelea mji wetu wakifurahia usiku wao wa Jumamosi," Khan alisema.
Trump azungumza na May
Rais donald Trump amempigia simu waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na kumpa rambi brambi zake kufuatia tukio la kigaidi mjini London.
Rais Trump alizungumza na waziri mkuu May leo na alitoa rambi rambi zake kwa shambulio hilo la kinyama la kigaidi katikati ya London.Trump aliahidi msaada kwa Uingereza kutokana na mashambulio hayo mawili ya kigaidi ambapo watu sita waliuwawa , baada ya gari kuwagonga wapita njia na washambuliaji hao kuwachoma visu watu kadha.
Katika mazungumzo yao ya simu Trump aliahidi kwamba Marekani itatoa ushirikiano kamili kwa Uingereza katika uchunguzi wa tukio hilo na kuwafikisha watu wanaohusika na tukio hilo la kiuwoga mbele ya sheria.
Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema kwamba wacanada , "wanasimama pamoja na Waingereza" baada ya washambuliaji kuwachoma visu holela watu na kuwagonga wapita njia kwa gari na kuuwa watu sita.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae /
Mhariri: Bruce Amani