Kibaki awaaga wana Afrika Mashariki
21 Februari 2013Kabla ya kuhitimisha ziara hiyo, Rais huyo wa Kenya alikuwa na mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake rais Jakaya Kikwete baada ya leo mchana kufungua bara bara iliyopewa jina lake.
Rais Kibaki ambaye aliambatana na ujumbe wa maafisa kadhaa, ametumia ziara hio kutoa shukurani kwa wananchi wa Tanzania ambao amewalezea kama marafiki wema kwa Kenya na amehaidi kuendelea kushirikiana nao hata atapoondoka madarakani baada ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika March 4.
Kwa heri Afrika Mashariki
Rais Kibaki ametumia jukwaa la Tanzania kutoa salamu za kwa heri kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kile kinachoelezwa kuwa kama moja ya agenda yake ya kutambua diplomasia yaTanzania ambayo ilifanikisha kumaliza mzozo uliozuka baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007.
Tamko kuhusu uchaguzi wa Kenya
Katika kikao na mwenyeji wake, Rais Kikwete, viongozi wote wawili wamezungumzia uchaguzi mkuu ujao wa Kenya na wakayataka madola ya magharibi kutoingilia kati kwa namna yoyote ile. Rais Kikwete hata hivyo ametaka kufanyika kwa uchaguzi wa haki na huru ili kuepuka hali yoyote ya sintofahamu.
Kwa upande wake rais Kibaki amasema kuwa yuko tayari kukabidhi madaraka kwa mgombea yoyote atayeshinda katika uchaguzi huo ambao unatupia macho na Jumuiya za kimataifa. Kuhusu uimarishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Mwai Kibaki alizitaka nchi wanachama kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa madai kuwa ndiyo lugha mama inayoweza kuwaunganisha wananchi wa eneo hili.
Sikiliza ripoti ya George Njogopa kutoka Dar es Salaam, kwa kubonyeza alama ya kusikiliza masikioni hapo chini.
Mwandishi:George Njogopa
Mhariri:Yusuf Saumu