1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Chavez cha uhuzunisha ulimwengu

6 Machi 2013

Washirika wa Venezuela wanamlilia Hugo Chavez wanaemtaja kuwa " Mtu wa aina pekee" na ambae kifo chake ni hasara isiyokuwa na kifani.

Hugo Chavez na binti yake Rosa VirginiaPicha: Reuters

Serikali ya kikoministi ya Cuba imetangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kumkumbuka mshirika wao mkubwa wa kisiasa na kiuchumi aliyelala miezi miwili hospitali kisiwani humo kabla ya kurejea nyumbani Caracas kati kati ya mwezi uliopita."Chavez pia ni Mcuba."Alikuwa akizijua kama sisi shida zetu na amefanya kila awezalo na,kwa ukarimu mkubwa,ameshirikiana na Fidel,kama mtoto wake wa kweli na alikuwa rafiki wa dhati wa Raul-taarifa ya serikali imesema mjini Havana.

Rais Barack Obama amesema Marekani inawaunga mkono wananchi wa Venezuela baada ya kifo cha kiongozi wao na kutaraji "uhusiano wa maana pamoja na serikali mpya ya nchi hiyo."Katika wakati ambapo Venezuela inafungua ukurasa mpya wa historia yake,Marekani itaendelea kuunga mkono vyama vya kisiasa vinavyounga mkono misingi ya kidemokrasia,taifa linalofuata sheria na haki za binaadam" amesema rais Barack Obama.Matamashi kama hayo yametolewa pia na waziri mkuu wa Canada Stephen Harper.

Katika bunge la Marekani Congress lakini wabunge wa Republican wamefurahikia kifo cha Hugo Chavez."Hugo Chavez alikuwa muimla aliyewafanya wananchi wake waishi katika hofu.Kifo chake kitaudhoofisha muungano wa viongozi wa mrengo wa shoto wanaoipinga Marekani katika Amerika ya kusini,amesema Ed Royce,ambae ni mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya baraza la wawakilishi la Marekani.

Hasara isiyokuwa na kifani

Hugo Chavez na rais Dilma Rousseff katika mkutano wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi na biashara ya Amerika Kusini-MERCOSURPicha: AP

Rais Evo Morales wa Bolivia,machozi yakimtiririka,,Rafael Correa wa Equador, Nicaragua,sauti ikitetemeka, Brazil ,Chili,na Colombia ambako Hugo Chavez amesaidia pakubwa katika utaratibu wa amani pamoja na wanamgambo wa FARC, kote huko viongozi wameelezea huzuni zao kwa msiba uliotokea.Rais Dilma Rousseff wa Brazil amesema hata kama Brazil haikuwa mara zote ikikubaliana na Hugo Chavez lakini kifo chake ni hasara kubwa isiyokuwa na kifani.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon amesifu juhudi za Hugo Chavez kukidhi mahitaji na changamoto za wasiojimudu nchini mwake."

Nchini Ujerumani waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle amesema kifo cha Hugo Chavez ni hasara kubwa kwa nchi hiyo ya Latin Amerika.Ameelezea matumaini ya kuiona Venezuela,baada ya siku za msiba na maombolezi ikichipukia katika enzi mpya.

Mwandishi:Hamidou OummilkheirAFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman