1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Helmut Kohl: Bendera zapepea nusu milingoti

17 Juni 2017

Bendera zinapepea nusu mlingoti katika jimbo la nyumbani kwa kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl, baada ya kifo chake kusababisha wimbi la salaamu za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Helmut Kohl Bad in der Menge
Picha: Picture-alliance/dpa/H. Hollemann

Kitabu cha rambirambi kwa ajili ya kiongozi huyo wa zamani wa Ujerumani, kitawekwa pia katika ofisi ya waziri mkuu wa jimbo la Rhineland-Palatinate kuanzia siku ya Jumapili na kuendelea, amesema msemaji wa serikali ya jimbo Andrea Baehner.

Waombolezaji wamekuwa wakiandika ujumbe wa kumbukumbu katika makao makuu ya chama chake cha Christina Democratic Union CDU, mjini Berlin, ambako kitabu kingine cha rambirambi kimefunguliwa.

Nyumbani, Kohl anakumbukwa juu ya yote, kama baba wa muungano wa Ujerumani, ambao ulipatikana baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin mwezi Novemba 1989. Alikonga nyoyo za wapigakura katika upande wa Ujerumani  ya kikomuniti ya Mashariki, kwa kuwaahidi maisha bora. Kifo chake kimepamba vichwa vya magazeti yote nchini Ujerumani kote hii leo.

Merkel amshukuru kwa kumjenga kisiasa

Kohl alimnasihi kansela wa sasa Angela Merkel, ambaye amesema binafsi anamshukuru kwa kazi kubwa alioifanya. Baada ya mazungumzo ya faragha na kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis mjini Vatican leo, Merkel alisema papa amemsifu Kohl kama kiongozi shupavu na mkereketwa wa Ulaya aliefanyakazi bila kuchoka kwa ajili ya umoja wa nchi yake na bara lake.

Mwanamke akiwasha mshumaa mbele ya nyumba ya marehemu Helmut Kohl katika wilaya ya Oggersheim, mjini Ludwigshafen, jimboni Rheinland-Palatinate Juni 16.06.2017.Picha: picture alliance/dpa/U.Anspach

Kohl alimjengea msingi wa uongozi Merkel, alipomtetua katika nafasi yake ya kwanza ya uwaziri.

"Helmut Kohl alikuwa Mjerumani na raia mshuhuri wa Ulaya. Urithi wa Helmut Kohl umeamua mambo mawili muhimu zaidi katika siasa zan Ujerumani katika kipindi cha miongo miwili iliopita: Kuungana upya kwa nchi,na kuungana kwa Ulaya. Helmut kohl alifahamu kwamba masuala haya mawili hayatwezi kutenganishwa."

Urithi mkubwa wa Helmut Kohl

Mwenyekit wa chama cha Social Democratic SPD, na mpinzani wa Merkel katika uchaguzi mkuu ujao Martin Schulz, amekitaja kifo cha Kohl kama hasara kubwa kwa Ujerumani na Umoja wa Ulaya pia.

"Helmut Kohl alikuwa mtu alieamua, na pia katika muktadha wa hadith ya maisha yake, kwamba Ujerumani inapaswa kuwa nchi y kiulaya na inapaswa kuunganishwa baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin," alisema Schulz.

"Aliiongoza kwa uthabiti nchi hii mpya - Jamhuri yetu ya shirikisho la Ujerumani - barani Ulaya. Kwake umoja wa Ulaya ndiyo ulikuwa mradi mkubwa zaidi wa uhuru na mafanikifio, na aliupigania kama kansela wa nchi yetu.

Mafanikio haya makubwa kama kansela wa Ujerumani, ya kuiongozea nchi yetu Ujerumani, ndiyo urithi mkubwa zaidi wa Helmut kohl kwa Ujerumani na Ulaya."

Naye mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF Christine Lagarde amemuelezea Kohl kama kiongozi mwenye maono aliejitolea zaidi kwa ajili ya urafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani pamoja na wazo la Ulaya ya amani na iliyoungana.

Wagombea wakuu wa nafasi ya kansela, Angele Merkel na Martin Schulz wamesema Ujerumani imepote mtu muhimu kutokana na kifo cha Kohl.Picha: picture-alliance/U. Baumgarten

Lagarde amesemani vigumu kuifkiria Ujerumani ilioungana bila dhamira ya Kohl isioyumbishwa kujenga madaraja kati ya masahriki na Magharibi. Amesema jina lake litahusishwa daima na kuimarika kwa Umoja wa Ulaya na kuundwa kwa sarafu ya pamoja ya Ulaya.

Die Mannschaft kuvaa utepe mweusi

Timu ya soka ya taifa ya Ujerumani itavaa utepe mweusi mikononi wakati wa mechi ya ufunguzi ya kombe la shirikisho ili kutoa heshima kwa kiongozi huyo.

Shirikisho la kandanda la Ujerumani limeliomba shirikisho la soka duniani FIFA, kuwaruhusu wachezaji wake kutoa heshima kwa Kohl wakati timu yao itakapocheza dhidi ya Australia mjini Sochi siku ya Jumatatu, katika mashindano ya maandalizi ya kombe la dunia mwaka 2018.

FIFA imethibitisha kwamba imeyakubali maombi ya Ujerumani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,ape

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW