Kifo cha Malkia Elizabeth chatawala magazeti ya Ujerumani
16 Septemba 2022Gazeti la Die Welt liliandika kuhusu ghadhabu ya Waafrika kufuatia kifo cha Malkia wa Uingereza Elizabeth wa pili. Kwa wengi alikuwa nembo ya ukoloni barani Afrika na kwa upande mwingine wataalamu wa sayansi ya siasa walikuwa na mitazamo tofauti. Mwandishi wa gazeti la Die Welt, Christian Putsch wa mjini Cape Town, Afrika Kusini aliandika kwamba mwitikio wa kinyongo zaidi labda ulikuwa wa Profesa wa isimu mzaliwa wa Nigeria Uju Anya kuhusu kifo cha Malkia Elizabeth II, akimtakia maumivu "ya kutisha" kwenye kitanda chake alichofia.
Anya aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akisema baada ya yote, malkia alikuwa na dhamana ya kuongoza ufalme ulioiba, kubaka, na kufanya mauaji ya kimbari." Mtandao wa Twitter uliifuta kauli hiyo muda mfupi baadaye, na mwajiri wake - chuo kikuu cha Marekani - kilijitenga mbali na tweet hiyo. Mhariri anasema Anya kwa upande mwingine, alipata uungwaji mkono wa kutia moyo, wakati tweet yake iliposambazwa na maelfu kwa maelfu ya watumiaji wa twita.
Nchi tajiri zilisaidie bara la Afrika
Gazeti la Handelsblatt liliandika kuhusu nchi tajiri kutakiwa kulisaidia bara la Afrika na mabilioni ya fedha. Mhariri wa gazeti hilo alisema vita nchini Ukraine na majanga kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yameliathiri mno bara hilo kwa kiwango kikubwa. Tajiri wa Marekani Bill Gates ametoa wito kutolewe msaada wa kilimo huku Wakfu wa Soros nao ukitaka msaada wa fedha utolewe kulisaidia bara la Afrika.
Gazeti la Handelsblatt lilisema mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa unakabiliwa na mijadala mikubwa muhimu. Nchi masikini zina matumaini ya kupata misaada zaidi kutoka kwa mataifa yaliyostawi kiviwanda, ambayo bajeti zao zimeathiriwa na kudhoofishwa na vita vya Ukraine na janga la virusi vya corona.
Muanzilishi wa kampuni ya Microsoft na mfadhili Bill Gates ameliambia gazeti la Handelsblatt kwamba nchi tajiri zinatakiwa zisaidie kilimo barani Afrika, bara ambalo linahangaika kutokana na athari za ukame na ukosefu wa chakula na bidhaa. Gates amenukuliwa na gazeti la Hendelsblatt akisema mataifa tajiri ndiyo yaliyosababisha tatizo hili kubwa ambalo tayari linaumiza uzalishaji wa kilimo wa bara la Afrika kutokana na viwango vya juu vya joto.
Ujerumani yakataa mazungumzo mapya kuhusu fidia na Namibia
Gazeti la Neues Deutschland lilikuwa na taarifa kuhusu Ujerumani kukataa kusikia maombi ya kufanya mazungumzo ya kudai fidia kutoka kwa jamii za Nama na Herero nchini Namibia. Upinzani wa Namibia unataka mazungumzo kuhusu makubaliano yaliyoafikiwa kuhusu mauaji ya kimbari ya Herero na Nama, lakini serikali ya shirikisho ya Ujerumani imelikataa pendekezo hilo ikitumia hoja za kisheria.
Mhariri wa gazeti la Neues Deutschland mjini Cape Town, Afrika Kusini, Christian Selz, anasema hatua hii imeibua chuki nchini Namibia. Anasema serikali ya Ujerumani haitaki kufanya mashauriano zaidi kuhusu tamko la pamoja na Namibia, makubaliano ambayo yaliafikiwa mnamo Mei 2021, kwa lengo la kulipa fidia kwa mauaji ya Herero na Nama yaliyofanywa na wanajeshi wa Ujerumani kuanzia 1904 hadi 1908 katika koloni la zamani la Ujerumani kusini magharibi mwa Afrika. Hata hivyo makubaliano hayo hayakuridhiwa kufuatia maandamano makubwa nchini Namibia.
Mjadala katika bunge la mjini Windhoek hatimaye ulikamilika bila matokeo yoyote kupatikana. Miungano ya mamlaka za jadi za Herero na Nama zilipinga vikali mkataba huo kwa sababu hawakuhusishwa katika mazungumzo. Mhariri anasema matumaini ya kupata makubaliano mapya na serikali ya shirikisho ya Ujerumani sasa yamezikwa.
Chanjo ya malaria yakaribia
Gazeti la Süddeutsche lilikuwa na taarifa kuhusu chanjo mpya ya malaria ambayo imedhihirika inafanya kazi. Mhariri wa gazeti hilo alisema chanjo mpya dhidi ya ugonjwa wa malaria huenda ikapatikana hivi karibuni, ikiwa mtafiti wa chuo kikuu cha Oxford Adrian Hill ataruhusiwa kupewa kibali. Gazeti limesema chanjo hiyo ya kwanza kabisa kuonyesha ufanisi huenda ikaidhinishwa mapema mwaka ujao. Siku ya Alhamisi, Hill na watafiti wengine kutoka nchini Uingereza na Burkina Faso walitangaza takwimu mpya kuhusu aina hiyo mpya ya chanjo.
Kwa mujibu wa ripoti chanjo hiyo inayoitwa R21 iliwakinga vyema zaidi watoto 80 waliochanjwa mara nne dhidi ya malaria wakilinganishwa na vijana waliochanjwa dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa. Awamu ya tatu na ya mwisho ya utafiti wa chanjo ya malaria itakayowajumuisha watoto 5,000 imeshaanza na inatarajiwa kukamilika mwaka ujao.
Pikipiki za kutumia betri
Boda boda bila mafuta: Ni kichwa cha habari cha gazeti la Frankfurter Allgemeine. Gazeti liliandika kuhusu raia wa Ufaransa Jason Gras na raia wa Ujerumani Emile Fulcheri kupeleka boda boda Afrika Mashariki, katika mradi ambao unategemea kikamilifu pikipiki zinazotumia betri zinazoweza kubadilishwa. Sasa wateja wameanza kutambua kwa sababu mzozo wa kimataifa kuhusu nishati unasababisha bei za mafuta kupanda. Hata hivyo mhariri anasema soko ni gumu.
Jason Gras amekuwa akiishi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi kwa miaka miwili. Miaka miwili iliyopita alianzisha kampuni yake kwa jina Stima pamoja na mshirika wake Emile Fulcheri wakitaka kuboresha usafiri wa boda boda nchini Kenya. Mhariri anasema boda boda ni mwanzo na kuna boda boda milioni 1.5 mjini Nairobi pekee, na pengine kiasi milioni 20 barani Afrika, kwa hiyo fursa ya biashara ni kubwa.
(Inlandspresse)