1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Kifo cha mwanaharakati polisi yakaliwa kooni Kenya

Shisia Wasilwa
9 Juni 2025

Idara ya Polisi nchini Kenya inamulikwa kwa kifo cha kutatanisha cha Mwalimu Albert Ojwang', aliyekuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii.

Maafisa wa polisi Kenya
Maafisa wa polisi KenyaPicha: Gerald Anderson/AA/picture alliance

Ojwang' alifia kwenye korokoro ya kituo kikuu cha polisi jijini Nairobi baada ya kukamatwa kwao katika jimbo la Homa bay kwa madai ya kuchapisha taarifa za uwongo kwenye mtandao wa X.

Kutokana na kifo hicho cha kutatanisha, Mkuu wa Polisi Douglas Kanja, amewasimamisha kazi maafisa wote waliokuwa kazini wakati wa tukio hilo. Maafisa hao ni pamoja na Mkuu wa Kituo Kikuu cha jijini Nairobi cha Polisi, afisa wa zamu na mlinzi wa korokoro.

Hatua hiyo inatoa nafasi kwa uchunguzi huru kufanywa na Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji wa Polisi (IPOA).

Ojwang, alikamatwa siku ya Jumamosi, tarehe 7 Juni mwaka huu, nyumbani kwao Kakot, Jimbo la Homa Bay na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai.

Inaripotiwa kuwa alikuwa anachunguzwa kwa madai ya kuchapisha taarifa ya uongo kupitia mitandao ya kijamii.

Alikuwa akila chakula cha mchana na babake Omondi Ojwang' kabla ya kutiwa pingu.

"Nikawauliza kwani amekosea nini, wakaniambia kijana wangu ametusi bosi wao vibaya sana katika X, huyo Sigei ndiye aliniambia ati ameharibu jina la mkubwa wake.” Alisema baba wa marehemu.

Kusafirishwa kwake hadi Nairobi

Baada ya kuzuiliwa awali katika Kituo cha Polisi cha Mawego, usiku wake alihamishiwa hadi Nairobi na kuwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi. Babake alikuwa akimfuata nyuma hadi Nairobi.

Polisi Kenya wakiwa wamevalia mavazi maalumPicha: Gerald Anderson/Anadolu/picture alliance

Kulingana na taarifa ya msemaji wa polisi, Muchiri Nyaga, Ojwang alipata majeraha kichwani na alipatwa akitokwa damu korokoroni.

Familia yake sasa inataka haki itendeke kwa mtoto wao. Kwa majonzi babake anasimulia jinsi mwanawe wa pekee alivyoaga dunia.

"Nimeambiwa kuwa Habari sio nzuri na kuwa mtoto wako alijigonga ukutani na amejiua.”

Mazungumzo kuhusu kifo cha Ojwang yameibua hisia kali miongoni mwa umma, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu, ikiwemo Amnesty International Kenya, yakilaani tukio hilo na kutaka uchunguzi wa kina.

Kwenye taarifa hiyo Mkurugenzi wa Amnesty International Kenya, Irungu Houghton, amesema kifo cha Ojwang' kilikuwa cha kusikitisha na kushangaza sana kuwa mtuhumiwa hakufikishwa katika kituo cha polisi cha karibu na alikamatwa na kusafirishwa mwendo mrefu hadi Nairobi.

Mashirika ya haki yataka hatua zichukuliwe

Chama cha Wanasheria nchini Kenya pia kimetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuhakikisha haki inapatikana. Faith Odhiambo ni Rais wa Chama hicho.

Wakati huyu kijana akiaga dunia, hatutaruhusu wahusika wajifiche, tutahakikisha kuwa mnachukua wajibu wa kitendo hicho, tunatarajia maafisa wakuu watakuja na kupata taarifa ya tukio hili.

Je, Polisi wapewe mafunzo maalumu kukabili maandamano?

02:46

This browser does not support the video element.

Mashirika ya kijamii yamepanga kufanya maandamano kupinga tukio hilo jijini Nairobi.

Kwa mara nyingine tukio hilo linapaka doa serikali ya Rais William Ruto ambayo imejipata ikikosolewa kwa mauaji ya kiholela ya wakosoaji wake.

Tukio hilo likijiri kipindi kifupi tu baada ya Rais kuwaomba msamaha vijana wa Gen Z kwa ukatili wa polisi dhidi yao. Haijafahamika wazi ni chapisho gani la uongo Ojwang alishutumiwa nalo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW