1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Mwanamuziki Moshi William wa Tanzania ni pengo kubwa katika ulimwengu wa Muziki

Christopher Buke2 Aprili 2006

Sauti yake ilikuwa ya kuvutia, alitunga nyimbo zenye hisia kali nyingi za tungo zake zilitokana na maswahibu ya maisha yake

Na Christopher Buke.

Wanamuziki wa Bendi ya Msondo ngoma wamesema kuwa pengo aliloliacha Mwanamuziki mwenzao TX Moshi William halitazibika kamwe.

Mwanamuziki huyu maarufu Tanzania na sehemu mbalimbali hasa Afrika Mashariki na ya kati aliaga dunia March 29, mwaka huu na kuzikwa siku hiyo hiyo katika makaburi ya Keko machungwa jijini Dar es salaam.

Ameacha mke na watoto watano, wawili wa kike na watatu wa kiume. Wanne wakiwa wa mama mmoja ambao ni Hassan, Maika, Ramadhani na Maada. Jina la motto mwingine bado halijafahamika.

Mwanamuziki huyo aliaga dunia siku ya Jumatano asubuhi majira ya saa tatu. Kwa mujibu wa Mke wa mwanamuziki huyo, Bi Asha Seif, William alikufa kutokana na kadhia ya mguu pamoja na figo.

Mguu huo ulivunjika katika ajali ya gari aliyoipata Desemba 16, mwaka jana, Februari 13, mwaka huu akalazwa Hospitali ya Burere Kibaha, baada ya mguu huo kuanza kumsumbua na kutunga usaha kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Regency Machi 15 baada ya kugundulika kuwa pia alikuwa na matatizo ya figo. Machi 18, alihamishiwa Muhimbili kwenye kitengo cha kushughulikia mifupa MOI.

Kwa mujibu wa Mmoja wa wanamuziki wa Bandi hiyo Bwana Saidi Mabera, Moshi William maarufu kwa jina la TX alijiunga na Kundi hilo mwaka 1982 akitokea Polisi Jazz.

Bwana Mabera aliiambia Izaa hii kuwa miongoni mwa nyimbo alizotunga mara baada ya kujiunga na bendi hiyo ni pamoja na Ajuza, Asha Mwanaseif, ( aliomtungia mkewe), na wimbo mwingine Ashibaye.

Anadai kuwa muimbaji huyo alitunga nyimbo nyingi baada ya kuhamia kwenye bendi hiyo lakini anasisitiza nyimbo zilizotia fora sana ni pamoja na Kilio cha Mtu Mzima, Ndoa Ndoana, Piga Ua Talaka Utatoa, Isihaka Kibene, Kaza Moyo, Harusi ya Kibene, na Ajali.

Wimbo huu Ajali aliutunga mara baada ya kupata ajali iliyompelekea kuvunjika mguu. Na ni mguu huo huo unaosemekana kusababisha mauti yake pamoja na ugonjwa wa figo.

Mara baada ya ajali hiyo na Mwanamuziki huyu kuonekana anapata nafuu baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania vilikariri wapenzi wa bendi hiyo ya Msondo mkoani Tanga wakidai kufanya tambiko maalumu ili kipenzi chao TX Moshi William apone na kuzidi kuwa na maisha marefu.

Lakini kama wasemavyo waswahili kuwa siku yake ilikuwa imefika, Moshi hatunaye tena. Ajuaye ni Mwenyezi MUNGU.

Bendi hii ya Msondo Muziki ilizaliwa kutoka Bandi ya OTTU ambayo pamoja na kubadilishwa jina mara kwa mara ilianzishwa mwaka 1964, ikiwa sehemu ya tawi la Chama cha wafanyakazi nchini National Workers Union.

Wakati huo ilipoanzishwa ilikuwa ikiitwa NUTA. Baadae jina hili likaja kubadilishwa na kuitwa Juwata Jazz Band mnamo mwaka 1977, na baadae kuitwa OTTU.

Mwanamuzi Said Mabera aliyefanya kazi kwa karibu na TX aliniambia kuwa kama kuna kitu ambacho kilimpa sana heba na heshima kubwa mwanamuziki huyu William ni uwezo wake wa kutunga na kuimba, tofauti na wanamuziki walio wengi ambao unaweza kukuta mwanamuziki anajua kuimba lakini hana uwezo wa kutunga nyimbo au ana uwezo wakutunga lakini hana sauti nzuri.

Hivi sasa bendi hii ilikuwa inamilikiwa na wanamuziki wenyewe na hivyo kubadilishwa jina kutoka OTTU jaz na kuwa Msondo Sound Music Band ikitumia mtindo ujulikanao kama Mambo Hadharani.

Bwana Moshi mwenyewe wakati wa uhai wake aliwahi kusema kuwa amepitia katika bendi mbalimbali za muziki ambazo ni pamoja na Safari Trippers, Juwata Jazz. UDA Jazz, na Polisi Jazz, ambayo alitokea wakati anajiunga na kundi hili.

Wakati wa uhai wake pia alijaliwa kupata tuzo mbalimbali za muziki hasa zile zijulikanazo kama Kilimanjaro Music Award.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania vinakariri kuwa Moshi alibatizwa jina la TX, na Mwandishi wa Habari wa siku nyingi aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania, Julius Nyaisanga. Vinadai vyombo hivyo kuwa Nyaisanga alimbatiza jina hilo kutokana na tunzi zake za uhakika. Kwa sasa Nyaisanga ni mtanzaji wa vituo vya radio na televisheni vinavyomilikiwa na kampuni ya IPP Media.

Mwimbajji huyu jina lake hasa ni Shaaban Mhoja Kishiwa ingawa amekuwa akijulikana zaidi kwa jina la Moshi William TX.

Alizaliwa mwaka 1958 Korogwe Tanga. Mengi hayafahamiki kwenye maisha yake inagawa wakati Fulani alikaririwa akisema kuwa hali hii ya kutotulia sehemu moja hasa wakati akiwa mtoto ilitokana na ugomvi baina ya Mama yake na Baba yake.

Miongoni mwa wanamuziki ambao tayari wameisha aga dunia na kuacha masikitiko makubwa katika ulimwengu wa muziki kutoka bendi hiyo ni pamoja na Suleiman Mbwembwe. Huyu naye alikuwa ana sauti nzuri na mara nyingi aliimba kwa kupokezana pamoja na William. Sasa wengi wanahoji nini mstakabali wa bendi hii ya Msondo Music band baada ya kuondokewa na majabari hawa wawili?

Kwa hakika Moshi William ameacha pengo kubwa ambalo halitazibika katika ulimwengu wa muziki wa Dansi Tanzania. Na kama alivyoniambia Bwana Waziri Dewa ambaye ni mratibu wa shughuli za Bandi hii ya Msondo, itakuwa kazi ngumu na isiyofikiriwa kumpata mwimbaji mwingine mwenye sauti yenye mvuto kama ya TX Moshi William.

Mwisho.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW