1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Odinga chaleta mshtuko na simanzi Kenya

16 Oktoba 2025

Wakenya wanaomboleza katika siku ya kwanza tangu taarifa za kifo cha marehemu Raila Odinga, kiongozi wa upinzani alipoaga dunia mapema hii leo. Kote nchini waombolezaji waliacha shughuli zao ili kumuenzi mwanasiasa huyo.

Majonzi Kenya baada ya Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga kuaga dunia
Wakenya washitushwa na kusikitishwa na kifo cha Raila Picha: Thelma Mwadzaya/DW

Wakaazi wa Kibra walijitokeza kwa wingi na kuelekea mtaani Karen kwenye makaazi ya marehemu Raila Odinga. Majonzi na simanzi ilihanikiza mtaani Karen kwenye makaazi ya marehemu waziri mkuu wa zamani nchini Kenya, Raila Odinga kufuatia taarifa za kifo chake mapema hii leo.Nyimbo za kuomboleza na vilio ndivyo vilivyosikika kutwa nzima.

Kufikia mchana,idadi kubwa ya waombolezaji wakiwemo wafuasi, wanasiasa na wakenya wa kawaida walifika Karen kwa ufariji.Wengi wamepigwa na butwaa na hawajaamini kuwa marehemu kigogo huyo wa upinzani amewaacha mkono.

Kwenye uwanja wa makaazi ya marehemu Raila Odinga, wakenya walibubujikwa na machozi na kukariri nyimbo za uokombozi ambazo ziliimbwa kwenye mihadhara ya siasa wakati wa uhai wake. Baadhi walikumbatia sala za ghafla wakiwa wamebeba picha za marehemu aliyetambulika na wengi kama Baba. Juhudi za familia za kuutuliza umati ziliambulia patupu. Gavana wa kaunti ya Homabay Gladys Wanga aliyewasihi waombolezaji kutulia hakufanikiwa.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir ambaye ni naibu mwenyekiti wa chama cha ODM alitoa rambirambi zake na kushindwa kujieleza kwa majonzi.

Wakenya washitushwa na kusikitishwa na kifo cha Raila Picha: Kevin Midigo/AFP

"Kabla nisafiri nilizungumza naye.Tukajadili mambo ya kawaida na alikuwa mcheshi,….amechangamka,…. ilikuwa muda tu baada ya safari ya Kasipul na Magarini.Nilimshauri atuachie mambo ya uchaguzi mdogo tushughulikie….alinipigia simu jana….

Raila aaga wakati chama chake kikitimiza miaka 20 katika siasa

Itakumbukwa kuwa chama cha upinzani cha ODM kinaadhimisha miaka 20 ya kushiriki katika siasa za Kenya. Mohamed Ali ni mbunge wa Nyali iliyoko kaunti ya Mombasa na amesikitishwa sana na kifo cha Raila Odinga na kumkumbuka kama mtetezi wa vijana.

"Alikuwa rafiki yangu kutoka zamani tulikuwa tunakutana mara kwa mara mnikiwa mwandishi.Na alikuwa anatupa motisha. Niliingia ODM ila mambo yalifanyika ambayo si vyema kuyazungumzia kwa sasa.Nilijiunga na kambi ya vyama binafsi na nikashinda. Halikumaliza uhusiano wangu na Raila.”

Giza limeshuka mtaani Karen nyumani kwa kiongozi huyo na biwi la simanzi limening'inia. Makundi ya wafuasi wanaomboleza baadhi kwa ibada na wengine kimyakimya wakitiririkwa na machozi kuashiria mwisho wa kipindi muhimu katika siasa za Kenya kwani marehemu Raila Odinga aliwania urais mara tano bila mafanikio.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW