1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo kutokana na Ebola chasababisha hofu Uganda

 Lubega Emmanuel12 Juni 2019

Hofu na mashaka vimewavaa wakaazi wa wilaya zinazopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia kifo cha kwanza cha raia wa Uganda asubuhi ya leo.

DR Kongo Butembo Beisetzung von Ebola-Opfern
Picha: AFP/J. Wessels

Wizara ya afya Uganda imetangaza hatua za dharura kukabiliana na mripuko wa Ebola ambao tayari umesababisha kifo cha mtoto mmoja huku watu wawili wakithibitishwa kuambukizwa. 

Hofu na mashaka vimewavaa wakaazi wa wilaya zinazopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia kifo cha kwanza cha raia wa Uganda asubuhi ya leo.

Lakini baadhi ya wakaazi hao wanazilaumu mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kutoimarisha juhudi za kukabiliana na maambukizi ya Ebola.

Wakaazi wa wilaya hizo ambao wakati mwingine husafiri nchini humo kwa shughuli za biashara na kuwatembelea jamaa zao, wamesema hawajawahi kuona vituo vya kupima wala kuhamasisha kama ilivyo kwa upande wa Uganda.

Kifo cha mtoto wa miaka mitano asubuhi ya leo pamoja na jamaa zake wawili waliokutwa na ugonjwa huo, akiwemo bibi yake mwenye umrri wa miaka 50, vimethibitsha kuwa mripuko huo umevuka mpaka kutoka DRC.Kwa muda wa miezi mitatu sasa Uganda imekuwa ikijiandaa kwa mripuko huo na mara tu kisa hicho kiliporipotiwa, serikali ilitangaza mara moja hatua za kuchukuliwa.

Waziri wa Afya nchini Uganda Jane Ruth Aceng, amesema waathiriwa wametengwa na umma ili wafanyiwe uchunguzi na wapate matibabu zaidi. 

Waganda watoa mwito kwa serikali kuzidisha juhudi za kupima watu wote na kuhamasisha umma kuhusu Ebola.Picha: Getty Images/A. Mcbride

Wakaazi na viongozi katika wilaya ya Buliisa na Kasese wamelezea kuwa wamefanya juhudi kubwa katika kuwadhibiti raia WaCongo wanaovuka mpaka na wana matumaini kuwa mripuko huo hautaiathiri Uganda kwa kiwango kikubwa.

Wakaazi wametoa mwito kwa serikali ya Uganda kuzidisha juhudi za kupima watu wote na kuhamasisha kuhusu Ebola.

Kulingana na takwimu za shirika la afya duniani WHO zaidi ya watu elfu moja wamefariki kutokana na Ebola nchini Congo na wengine zaidi ya 2,000 wamepimwa na kutibiwa.

Shughuli za chanjo zinaendelea sehemu mbalimbali lakini ukosefu wa usalama na amani vimechangia pakubwa katika kutatiza juhudi zao. Wakati mwingine wapiganaji wamewashambulia wahudumu wa afya.

Uganda inasema itaendesha zoezi kabambe la kutoa chanjo kuanzia tarehe 14 kwenye maeneo yanayopakana na DRC.