Kigali washangilia kuondoshwa vikwazo vya corona
8 Februari 2021Kuondolewa kwa vizuizi hivyo kumekuja baada ya kujitokeza upinzani mkali wa wananchi kupitia mitandao ya kijamii, wakiwatuhumu viongozi kutotilia maanani maslahi ya mwananchi wa tabaka la chini wakati wa kuchukuwa maamuzi kama hayo.
Hali ya afueni imedhihirika wazi kwa maelfu ya wakaazi wa Kigali walioruhusiwa kuingia mitaani tena leo kufafuta riziki, baada ya kujifungia ndani kwa takribani wiki tatu, wakiheshimu maelekezo ya serikali ya kudhibidi kasi ya maambukizi ya COVID-19. Jana Jumapili ulikuwa mwisho wa siku saba za nyongeza za kufungwa shughuli zote za kiuchumi, isipokuwa zile za msingi tu, katika juhudi za kuzuia kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Felix Shema anasema hakika maisha yalikuwa magumu mno. Alikiri hayo wakati alipozungumza na idhaa hii. "Kwa kweli madhara ya lockdown ni makubwa sana, sana sana kwa sisi wenye kipato cha chini, haiwi rahisi kwa sababu tunakula kama tukitoka tukaenda kutafuta, kwa hiyo katika muda huu wa lockdown nyumba nyingi tulikuwa tunakula mara moja kwa siku.”
Kulianza kusikika malalamiko hasa kupitia mitandao ya kijamii baada ya tangazo la kuendelea kufungwa kwa shughuli kwa siku siku saba za nyongeza lililotolewa kufuatia kikao cha baraza la mawaziri tarehe 2 mwezi huu wa Februari, huku baadhi ya wakaazi wakiwashutumu mawaziri wenye mshahara wa kila mwezi kutowajali watu wanaoishi kwa kutegemea vibarua, ambao sharti watoke nje ili kupata mlo wao.
Ingawa serikali ilitoa chakula kwa wasionacho, wapo walionekana katika mitandao hiyo wakisema wamebaguliwa na misaada haikuwafikia, huku waliopata msaada huo pia wakisema haukuwa wa kutosha, kama anavyosema Maureen, "Maskini hapa waliteseka, walipewa chakula kweli wakapewa unga na maharage lakini utapewa unga bila mafuta wala chumvi utakulaje? Bila sukari watoto watakunywaje uji?”
Kwa upande mwingine lakini wapo ambao wanaisifu serikali kwa hatua kali ilizozichukuwa kupambana na COVID-19 wakisema iliwapanua kiakili. Huyu hapa ni Vital Karangwa ambaye pia alizungumza na DW Kiswahili. "Lockdown imetufanya watu kubadili mtindo mzima wa maisha, kwa mfano imetulazimisha kujifunza kutumia teknolojia, kutumia pesa kwa uwajibikaji, kuzingatia sheria na kadhalika.” Tizama Video
Naibu waziri wa Afya Dr Mpunga Tharcisse amesema masharti yaliyowekwa kudhibiti kasi ya kuenea kwa virusi vya corona yamefikia malengo yake. Alisema "Takwimu zinaonesha idadi ya visa vya maambukizi imeshuka wiki tatu zilizopita nchini kote toka watu 367 hadi takribani 150 kwa siku, huku mjini Kigali ikishuka toka 200 hadi 50.”
Pamoja na mafanikio hayo serikali imeshauriwa kuhakikisha inatoa misaada ya kutosha endapo itabidi kutangazwa marufuku nyingine ya watu kutotoka nje ili mapungufu yaliyotokea yasijirudie.
Kando ya wakaazi wa Kigali kuruhusiwa kutoka nje kuanzia leo wameruhusiwa pia kwenda mikoani huku wakazi wa mikoani nao wakiruhusiwa kuja mjini Kigali.
Janvier Popote- Kigali