1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kigeugeu cha Trump Mmagazetini

Oumilkheir Hamidou
18 Julai 2018

.Kigeugeu cha Donald Trump, na matamshi yake makali dhidi ya nchi za Umoja wa Ulaya na pia Madiba na hali namna ilivyo miaka 24 tangu rais wa kwanza mweusi kuingia madarakani Afrika Kusini magazetini

USA, Washington: Trump kommentiert das Treffen mit Putin im US-Kongress
Picha: picture-alliance/O. Douliery

.

Tunaanzia Marekani ambako rais wa nchi hiyo yenye nguvu zaidi ulimwenguni Donald Trump anakosolewa tangu na wapinzani wake mpaka na wafuasi wake. Chanzo ni yale matamshi ya kutatanisha aliyoyatoa alipokutana na kiongozi mwenzake wa Urusi katika mji wa Helsinki nchini Finnland. Gazeti la Passauer Neue Presse linaandika: " Donald Trump amevunja rekodi nyengine. Hakuna rais yoyote mwengine kabla yake, aliyefanikiwa kuwafanya takriban wanasiasa wa vyama vyote wachukizwe nae, kama yeye. Hadi wakati huu watu walikuwa wakijiuliza wanaopigania uzalendo nchini Marekani watavumilia mpaka lini kumuona rais wao, Donald Trump akijiaibisha kila mara yeye binafsi na nchi yake ulimwenguni. Fadhaa ya Helsinki imegeuka lile tone la maji lililopelekea mtungi kufura. Tutegemee tu kwamba hamaki hizi za sasa hazitafifia na badala yake zitageuka motisha ya kupitishwa hatua za kisiasa. Rais aliyepokonywa imani ya wananchi kwa wingi kama huyo baada ya kumpigia magoti Putin, hastahiki kuendelea kuwepo madarakani.

Mkamia maji hayanywi

Na sasa tunaugeukia upande wa kibiashara ambao pia rais wa Marekani Donald Trump anaweka mhuri wake kwa kutangaza ushuru kuwaadhibu wale ambao hadi wakati huu walikuwa washirika wakubwa wa nchi yake. Akiwa ziarani barani Ulaya wiki iliyopita rais huyo wa Marekani alifika hadi ya kuwataja wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwa ni "maadui wa nchi yake". Nini wafanye basi nchi za Umoja wa ulaya kama si kusaka njia ya kunusuru biashara huru. Gazeti la  "Frei Presse" linamulika makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja wa ulaya na Japan na kuandika: "Sera za kujipendelea zinazofuatwa na rais Donald Trump zinaonyesha kugeuka fursa njema ya kuendelezwa fikra ya biashara jumla na huru ulimwenguni. Hilo bila ya shaka Donald Trump silo alilolikusudia. Kwa hivyo Trump anabidi atahadhari asije hatimae akaondolewa patupu katika biashara ya dunia. Ikiwa uchumi wa Marekani utadorora kutokana na hatua za kujikinga na kujipigania, huku ule wa sehemu iliyosalia ya dunia ukinawiri kutokana na biashara huru,Trump atatambua  hapo kwamba kauli mbiu "America First" haikuwa fikra nzuri."

Urithi wa Mandela ukoje Afrika Kusini

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Afrika Kusini ambako mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung anamulika hali namna ilivyo  miaka 24 baada ya kumalizika enzi za ubaguzi wa rangi na mtengano. Gazeti linaandika: "Afrika Kusini mpya ni nchi ya kuvutia kupita kiasi, lakini haikukamilika na hakuna usalama. Nelson Mandela asingependezewa hata kidogo na hali namna ilivyo hivi sasa nchini Afrika Kusini. Rais Cyril Ramaphosa anajitahidi kupambana na rushwa miongoni mwa wafuasi wa chama chake. Lakini anaonyesha kufuata utaratibu unaotisha wa kugawanywa ardhi. Anaashiria, wazungu wapokonywe ardhi na wapatiwe waafrika bila ya kulipwa fidia-kama katiba inavyosema. Mandela angekuwa hai asingekaa kimya. Sio kwasababu ya kuwapendelea wazungu bali kwaajili ya kuheshimu haki. Maovu ameyaona, lakini amesamehe.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga