1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kigoma: Kwa nini wahanga wa ukatili wa kijinsia hukaa kimya?

29 Aprili 2026

Licha ya kuenea kwa ukatili wa kijinsia katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania, wahanga wengi hukaa kimya kutokana na hofu, mila na ukosefu wa elimu, hali inayokwamisha juhudi za kupambana na tatizo hilo.

Tanzania, Kasulu 2026 | Rebecca Rocky akiwa na watoto walioathiriwa na ukatili
Rebecca Rocky Mwanaharakati wa utetezi wa haki za jinsia akiwa na watoto waliokutwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na uwepo wa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika kaya zao mjini kasulu mkoani KigomaPicha: Prosper Kwigize

Katika Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine nchini Tanzania, ukatili wa kijinsia (GBV) bado umeenea licha ya jitihada mbalimbali za kuudhibiti. Hata hivyo, changamoto kubwa ni kwamba matukio mengi hayaripotiwi, huku wahanga wakichagua kukaa kimya.

Ripoti za Benki ya Dunia, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonyesha ukubwa wa tatizo hilo. Kigoma inashika nafasi ya saba kwa asilimia 61 ya visa, huku Shinyanga ikiongoza kwa asilimia 78, na Kaskazini Pemba ikiwa na kiwango cha chini cha asilimia 8.

Afisa Ustawi wa Jamii mjini Kasulu, Tausi Baraka, anafafanua kuwa ukatili wa kijinsia ni ukatili unaofanywa kwa mtu kwa misingi ya jinsia yake, ukiwemo pia dhidi ya watoto.

Anaeleza kuwa ukatili huo hujitokeza kwa namna mbalimbali, ikiwemo vipigo (kimwili), kunyimwa haki ya kiuchumi, pamoja na ukatili wa kingono.

Hata hivyo, kuelewa aina hizi za ukatili ni hatua muhimu katika kuhamasisha jamii kutoa taarifa na kusaidia wahanga.

Rebecca Rocky akiwa na watoto wanaolelewa katika kituo cha collective calling Kasulu; watoto wengi hutelekezwa na wazazi kutokana na ukatili majumbani, na hivyo kuhitaji misaada ya kiutu na kijamii nje ya kaya zao,Picha: Prosper Kwigize

Maafisa wa ustawi wa jamii wanasema sababu kuu zinazochangia ukimya wa wahanga ni pamoja na hofu ya jamii, mila potofu na ukosefu wa uelewa.

Afisa mwingine wa ustawi wa jamii, Managwa Boaz, anasema mwamko bado ni mdogo na hata ndugu wa wahanga huogopa kutoa taarifa kwa hofu ya migogoro au mamlaka.

Aidha, matumizi mabaya ya teknolojia na mabadiliko ya kijamii pia yanatajwa kuchangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili.

Kwa mujibu wa wadau, elimu kwa jamii—hasa kwa wanaume—inaweza kusaidia kubadili mitazamo na kupunguza matukio ya ukatili.

Ufuatiliaji wa madawati ya jinsia na ushuhuda wa manusura unaonyesha kuwa msaada upo, lakini hauwafikii wengi kutokana na ukimya huo.

Picha hii inaonyesha maandamano ya kitaifa dhidi ya ukatili wa kijinsia (GBV) mjini Lusaka, Zambia, hali inayoashiria kuenea kwa tatizo hilo zaidi ya Kigoma.Picha: NGOCC Media Team

Wanaume pia waathirika

Mratibu wa kituo cha watoto walio katika mazingira magumu, Rebeca Rocky, anasema si wanawake pekee wanaoathirika, bali hata wanaume hukumbana na ukatili lakini hukaa kimya.

Anabainisha kuwa wanaume wengi hushindwa kuzungumzia changamoto wanazopitia majumbani, hasa pale wanapokosa uwezo wa kiuchumi.

Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ndio wanaoathirika zaidi, ingawa wanaume pia wanaguswa na tatizo hilo.

Katika mwaka 2022–2023, visa 37,448 viliripotiwa kwa wanawake na 30,566 kwa wanaume.

Wadau wanasema hatua muhimu ni kuongeza elimu kuanzia ngazi za chini ili watoto na jamii kwa ujumla waweze kutambua na kupinga ukatili.

Wanawake wanaopambana na ukatili wa kijinsia barani Afrika

04:09

This browser does not support the video element.

Suluhisho na mwito wa kuchukua hatua

Wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kuvunja ukimya kwa wahanga ili waweze kupata msaada wa kisheria na kijamii.

Elimu ya mapema kwa watoto kuhusu ukatili na namna ya kujilinda inatajwa kuwa njia muhimu ya kuzuia tatizo hilo kwa muda mrefu.

Aidha, jamii inahimizwa kushirikiana na mamlaka ili kuhakikisha wahanga wanapata haki zao.

Kwa ujumla, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa jamii, serikali na wadau wa maendeleo ili kupunguza matukio na kusaidia waathirika.

Mwito mkubwa unabaki kuwa mmoja—kuvunja ukimya na kuzungumza ili kupata msaada.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW