1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaQatar

Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh azikwa

2 Agosti 2024

Maelfu ya waombolezaji walikusanyika Ijumaa kwenye msikiti wa Imam Mohammad Abdul Wahhab mjini Doha kumsalia na kumzika aliyekuwa kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh aliyeuawa siku ya Jumatano nchini Iran.

Ismail Haniyeh aliuawa katika shambulizi la anga nchini Iran
Swala ikiendelea mbele ya majeneza ya aliyekuwa kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh na mlinzi wake katika msikiti wa Doha, nchini QatarPicha: Qatar TV/AP/dpa/picture alliance

Shughuli ya kumsalia ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Qatar na mataifa ya Kiarabu. 

Jeneza la Ismail Haniyeh, lililokuwa limefunikwa bendera ya Palestina lilibebwa kwa uangalifu mkubwa wakati likiingizwa msikitini na wakati likiondolewa. Maelfu ya waombolezaji waolifurika ndani na nje ya msikiti huo mkubwa kabisa nchini Qatar wa Imam Mohammad Abdul Wahhab walishiriki shughuli hiyo kwa uvumilivu baada ya swala ya Ijumaa. Wengine walilazimika kukaa nje kwenye mikeka, ambako joto lilifikia nyuzijoto 44C.

Soma pia: Qatar yafanya shughuli ya kumzika kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh

Miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu waliohudhuria, ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Reza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan. Uturuki na Pakistan yametangaza hii leo kuwa siku ya kitaifa ya kumuomboleza Haniyeh huku Hamas wakiita leo kuwa ni "siku ya ghadhabu kali".

Kwa mujibu wa Hamas, mwili wake ulipelekwa hadi mji wa Lusail kaskazini mwa Doha ambako amezikwa na ni familia yake tu ndio iliyohudhuria.

Mmoja ya waombolezaji ambaye ni mwanafunzi anayesoma Jordan, lakini anayeishi Doha Taher Adel alisema Haniyeh alikuwa nguzo na kiongozi wa mapambano. Na watu wamekasirishwa na kifo chake.

Ismail Haniyeh anatajwa kuwa nguzo muhimu na kiongozi wa mapambano na siku zote atakumbukwa kwa kuwa na misimamo thabitiPicha: Iran's Presidency /WANA/REUTERS

Mmoja ya wafuasi wa wanamgambo wa Houthi Abdo Quad Yusuf alisema "Ujumbe wetu kwa mataifa ya Kiarabu ni kwamba watufungulie mipaka. Watu wa Yemen wako tayari kutembea kwa miguu kwenda kupambana dhidi ya Israel. Tutakwenda na chakula na vinywaji vyetu.. hatutaki watupe chochote. Majibu yatakuja mara moja, na yatakuwa mabaya kwa Wayahudi na Marekani." 

Soma pia:Khamenei aongoza sala ya jeneza la Haniyeh

Haniyeh, aliyekuwa akiishi uhamishoni Qatar pamoja na familia yake aliuawa siku ya Jumatano akiwa mjini Tehran, Iran kufuatia shambulizi la anga ambalo pia lilimuua mlinzi wake.

Haniyeh amekuwa kiongozi wa muda mrefu wa kundi la Hamas na kiungo muhimu sana katika juhudi za kimataifa za kujaribu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano katika mzozo unaoendelea huko Ukanda wa Gaza na mabadilishano ya mateka wanaozuiwa kwenye magereza ya Israel.

Na huko Jerusalem, taarifa zinasema Israel imemuita balozi wa Uturuki kutoa maelezo baada ya kupandisha bendera nusu mlingoti katika jengo lake la mjini Tel Aviv, ikimuomboleza Haniyeh.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Israel Katz amesema kwenye taarifa kwamba taifa hilo halitavumilia ishara yoyote ya maombolezo ya kiongozi huyo wa Hamas. Lakini Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki alimjibu Katz kupitia X kwamba  "Israel haitafanikiwa kupata amani kwa kuwaua wapatanishi na kuwatisha wanadiplomasia."

Soma pia: UN yapinga wapalestina kuhamishwa Gaza

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW