1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir na Machar waahidi amani na maendeleo Sudan Kusini

9 Julai 2021

Wanasiasa wawili walio na nguvu Sudan Kusini wamesema hawatolirudisha taifa hilo katika vita. Wameyasema hayo wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya Uhuru wa taifa hilo changa kabisa duniani.

Südsudan Salva Kiir und Riek Machar | Entscheidigung für  Einheitsregierung
Picha: AFP/A. McBride

Katika hotuba yake ya siku ya uhuru, rais Salva kirr amewahakikishia raia wake kuwa hatowarejesha tena katika vita, huku akitoa wito wa kufanya kazi kwa pamoja ili kuirejesha nchi katika ukurasa mpya wa maendeleo.

Naye mwenzake Riek Machar, akizungumza mjini Juba amesema yeye na Kiir wanashirikiana na wanatarajia kuwa na majibu mazuri kuelekea amani.

soma zaidi:Vurugu zimeendelea Sudan Kusini licha ya mkataba wa amani

"Watu wetu wanatarajia mambo mengi kutoka kwetu, dunia pia inatarajia mengi kutoka kwetu. Ili kuendelea kusherehekea siku ya uhuru wakati wote, ni lazima tusimamie masuala ya amani," alisema Machar.

Papa Francis awataka viongozi wa Sudan Kusini kujitolea kufikia amani ya kudumu

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis Picha: Stefano Spaziani/picture alliance

Kwa upande wake kiongozi wa kanisa duniani Papa Francis amewaambia viongozi hao wawili waweke juhudi zaidi kufikia amani ya kudumu na kuwaahidi kulitembelea taifa hilo ambalo kulingana na ripoti za Umoja wa Mataifa mapigano bado yanaongezeka katika baadhi ya maeneo.

Katika taarifa ya pamoja na viongozi wengine wa kikristo, Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby na msemaji wa kanisa la Scotland Jim Wallace, Papa Francis anayepata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa utumbo, amesema ni jambo la kusikitisha kwa raia wa Sudan Kusini kuendelea kuishi kwa hofu na mashaka.

soma zaidi: Sudan Kusini yaadhimisha miaka 10 ya uhuru

Amesema ili kuwa na amani, viongozi hao ni lazima wajitolee kwa hilo.

Kiir, Machar na wanasiasa wengine kwa kikristu walialikwa katika makao makuu ya Vatican mwaka 2019 ambako Papa Francis alipiga magoti chini ya miguu yao na kuwaomba kutorejea tena katika mapigano.

Mgogoro uliibuka nchini Sudan Kusini mwishoni mwa mwaka 2013 miaka miwili baada ya kujitenga na Sudan, wakati rais Kiir  anayetokea kabila la Dinka alipomfuta kazi Riek Machar kama makamu wake wa rais anaetokea kabila hasimu la  Nuer.

Miaka 10 ya Uhuru wa Sudan Kusini

01:33

This browser does not support the video element.

Baadae wawili hao walitia saini makubaliano kadhaa ya kumaliza mapigano hayo yaliyochochewa na tatizo la muda mrefu la kikabila, yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu 400,000 na hatimaye kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka uliyopita.

Kiir alilivunja baraza lake la mawaziri mwezi Mei ili kutoa nafasi kwa baraza pana zaidi lililowajuisha wabunge 550.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters