Kiir:Makubaliano ya nchi za Sudan yatekelezwe haraka
26 Januari 2013Akizungumza katika mkutano wa usalama mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kiir amesema ni lazima waache maneno matupu na kuanza kufanya vitendo. Kiir na rais mwenzake wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, walikutana mapema jana Ijumaa kwa mazungumzo ya ana kwa ana katika hatua ya kushinikiza utekelezwaji wa makubaliano yaliyokwama ya kiuchumi, mafuta na usalama, yaliyosainiwa mwezi Septemba mwaka jana, baada ya kuzuka kwa mzozo katika eneo la mpakani mwaka uliopita.
Masuala mengine yaliyokwama
Masuala mengine muhimu ambayo bado hayajatatuliwa tangu Sudan Kusini ijipatie uhuru wake Julai mwaka 2011, ni pamoja na mkoa wenye mgogoro wa Abyei, pamoja na kuratibu uchimbaji wa mafuta. Jopo la upatanishi la Umoja wa Afrika-AUHIP limewasilisha azimio kuhusu Abyei, ambalo linajumuisha kura ya maoni inayowapa uwezo kabila la Dinka linaloishi Abyei, haki ya kupiga kura sambamba na raia wengine wa Sudan.
Rais Kiir ameitaka Sudan kuzingatia pendekezo la Umoja wa Afrika kuhusu Abei kwa lengo la kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu sasa. Amesema suala la Abyei ambalo limedumu kwa miaka saba sasa, halihitaji tena majadiliano, bali kinachotakiwa ni kutekelezwa kwa azimio la umoja huo. Akijibu swali iwapo kuna mafanikio yoyote kutokana na mazungumzo yake na Rais Bashir, Rais Kiir amesema bado hawajamalizana.
Lamamra auzungumzia mzozo wa Sudan
Aidha, Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra amesema umoja huo una wasiwasi kwamba tofauti kubwa bado imebakia kati ya mataifa hayo mawili hasimu. Lamamra amezitaka nchi hizo kushinikiza upatikanaji wa muafaka katika kutekeleza makubaliano hayo yaliyokwama. Sudan na Sudan Kusini zimekuwa zikitupiana lawama, ambapo Sudan imeishutumu Sudan Kusini kwa kuwafadhili waasi wa Sudan, jambo ambalo limesababisha kushindwa kutekelezwa kwa makubaliano hayo. Ama kwa upande wake, Sudan Kusini inaishutumu Sudan kwa kuwaunga mkono wanamgambo nchini humo, ikiwa ni njama iliyoitumia kufanya mashambulizi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo miwili.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Sekione Kitojo