Kijana aaminika kujiua Malaysia baada ya swali la Instagram
16 Mei 2019Mkuu wa polisi wa wilaya Aidil Bolhassan aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 na ambaye hakutajwa jina aliwataka wafuasi wake wamsaidie kuamua jambo alilotaja kuwa la 'muhimu sana', kuchagua ikiwa anapaswa kujiua au kuishi, saa kadhaa kabla ya kujirusha kutoka kwenye paa eneo la Sarawak, mashariki mwa Malaysia siku ya Jumatatu.
Afisa huyo wa polisi alieleza zaidi kuwa washiriki walipaswa kuchagua herufi 'D' kumaanisha 'Death' yaani kifo au 'L' kumaanisha 'Life' yaani uhai. Asilimia 69 ya waliojibu swali hilo walichagua D yaani kifo.
Bolhassan alisema wanafanya uchunguzi kubaini ikiwa kulikuwa na masuala mengine ambayo yalichangia kifo chake, huku akiongeza kuwa msichana huyo alikuwa na historia ya msongo wa mawazo.
Msemaji wa mtandao wa Instagram nchini Malaysia Serena Siew amesema waliufuatilia ukurasa wa msichana huyo pamoja na swali alilouliza ambalo lilimalizika baada ya saa 24 na wakabaini kuwa mwisho wa yote asilimia 88 walioshiriki walichagua L yaani kumtaka aishi. Hata hivyo Aidil ameeleza huenda matokeo ya kura hiyo yalibadilika baada ya habari ya kifo chake kusambaa.
Waliochagua jibu la kifo walaumiwa
Kisa hicho kimezusha wasiwasi miongoni mwa wabunge wa Malaysia wanaotaka uchunguzi utanuliwe.
Ramkarpal Sing ambaye ni wakili na mbunge, amesema wale waliopiga kura ya kumtaka msichana huyo ajiue, wanaweza kuwa na hatia ya kusaidia mtu kujiua.
"Lau wafuasi wengi wa wafuasi wake kwenye mtandao wa Instagram wangemhimiza kuishi na kuepukana na mawazo ya kujiua, si angekuwa hai leo”? Wakili Sing ameuliza kwenye taarifa yake na kueleza kuwa labda angetafuta ushauri wa kitaalamu kwa kufuata ushauri wa wafuasi wake.
Waziri wa vijana na michezo Syed Saddiq Abdul Rahman poa ametaka uchunguzi ufanywe akisema kuongezeka kwa visa vya watu kujitoa uhai na matatizo ya akili miongoni mwa vijana vyapaswa kushughulikiwa kikamilifu.
Shinikizo laongezeka kwa kampuni za mitandao ya kijamii kuhakikisha usalama wa watumiaji
Kulingana na sheria za Malaysia, yeyote anayepatikana na hatia ya kusaidia mtoto kujiua anaweza kuhukumiwa kifo au kifungo cha hadi miaka 20 jela pamoja na faini.
Mtandao wa Instagram umewapa pole familia ya mwendazake na kusema ni wajibu wa mtandao kuhakikisha watumiaji wake wako salama na wanasaidiwa.
Ching Yee Wong ambaye ni mkuu wa mawasiliano wa Instagram kanda ya Asia-pasifiki amesema kama sehemu ya juhudi zao wenyewe, wanawahimiza watumiaji wao wote kuripoti ikiwa wameshuhudia ujumbe au posti inayohatarisha usalama.
Mnamo mwezi Februari, mtandao wa Instagram ulipiga marufuku picha na ujumbe wa watu kutaka kujidhuru.
Hatua hiyo ilijiri baada ya shinikizo kutoka kwa wazazi wa kijana mmoja wa Uingereza aliyeamini kuwa kwa kutizama kurasa za Instagram zenye picha au ujumbe wa kujidhuru na msongo wa mawazo kulichangia msichana wao kujiua mwaka 2017.
Chanzo: Reuters