Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chaanza
19 Septemba 2017Mambo yanayomulikwa zaidi katika kikao cha mwaka huu ni mgogoro wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini, mauaji ya waislamu Myanmar na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Baraza hilo la siku sita, linafunguliwa leo huku Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa , Antonio Gutteres akitarajiwa kutoa hotuba yake ikiwa ni mara yake ya kwanza kuhudhuria baraza hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Gutterres alisema kikubwa atakachozungumza katika baraza hilo ni mgogoro wa Korea Kaskazini, mgogoro wa Myanmar na mabadiliko ya tabia nchi. Alisema mgogoro wa Korea Kaskazini ni miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa.
Ingawa Rais wa China Xi Jinping hatahudhuria baraza hilo lakini Rais Trump alizungumza naye kwa njia ya simu kuhusu ulazima wa kulitumia baraza la usalama la umoja wa mataifa kutafuta suluhu kwa kuishinikiza Korea Kaskazini kuacha matumizi ya silaha za kinyuklia.
Kadhalika katika mkutano huo, viongozi wengi wanahofia kuhusu nafasi na wajibu wa Marekani duniani na watapata nafasi ya kukutana na kumsikia Donald Trump ambaye anatajwa kuwa ni mgeni katika masuala ya kidiplomasia.
Pia hotuba yake inatarajiwa kuupiga zaidi Umoja wa Mataifa kwani tayari katika hotuba zake za awali mara baada ya kufika New York ameanza kuuponda akisema kuna urasimu na kurejea wito wake wa kufanyika mageuzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya baraza hilo, mara baada ya Gutteres kutoa hotuba yake ya ufunguzi, atafuatia Rais wa Brazil, Michel Temer na baadaye Donald Trump.
Wengine watakaohutubia ni pamoja na Mfalme wa Qatar Sheikh Tamin bin Hamad Al-Thani ambaye nchi yake inatuhumiwa kushirikiana na makundi ya kigaidi, wengine ni Rais wa Uturuki, Recep Tayip Edrogan na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Mada nyingine zinazotarajiwa kujadiliwa katika baraza hilo ni migogoro katka nchi za Venezuela, na Syria na mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi kama al-Qaida na Dola la Kiislamu.
Mwandishi: Florence Majani, AFP,AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman