1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha bunge chaahirishwa Iraq

1 Julai 2014

Wabunge waliochaguliwa karibuni nchini Iraq walikutana leo(01.07.2014),wakiwa katika mbinyo wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuepusha nchi hiyo kugawanyika baada ya mashambulizi ya Waislamu wenye Imani kali.

Nuri al-Maliki Ministerpräsident Irak
Waziri mkuu Nuri al-MalikiPicha: picture-alliance/dpa

Wapiganaji hao wametangaza taifa litakaloongozwa na Khalifa , na kuwaongoza Waislamu wote duniani.

Hata hivyo kikao hicho kimeahirishwa na kitaitishwa tena katika muda wa wiki moja ijayo.

Wakati huo huo Marekani inapeleka wanajeshi wengine 300 nchini humo kuimarisha usalama katika ubalozi wake na kwingineko mjini Baghdad kuwalinda raia wa Marekani na mali zao.

Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-MalikiPicha: AFP/Getty Images

Maliki mashakani

Kikao cha bunge jipya katika eneo la Baghdad lenye ulinzi mkubwa la ukanda wa kijani, kilitarajiwa kufikisha mwisho utawala wa miaka minane wa waziri mkuu kutoka jamii ya Washia Nuri al-Maliki, ambapo mahasimu wamedhamiria kumuondoa madarakani na hata baadhi ya washirika wake wakisema anahitajika kuondolewa na mahali pake pakachukuliwa na mtu ambaye hasababishi mtengano kwa kiasi kikubwa.

Majeshi ya Iraq yamekuwa yakipambana kwa wiki tatu dhidi ya wapiganaji wanaoongozwa na kundi ambalo hapo kabla lilikuwa linajulikana kama Taifa la Kiislamu nchini Iraq na Sham (ISIL).

Mapigano yameendelea katika siku za karibuni katika mji anakotoka kiongozi wa zamani wa nchi hiyo dikteta Saddam Hussein wa Tikrit.

Kundi la ISIL, ambalo linatawala maeneo kutoka Aleppo nchini Syria hadi karibu ya eneo la mji mkuu wa Iraq , Baghdad, limebadilisha jina na kujiita Taifa la Kiislamu. Limemtangaza kiongozi wao , mpiganaji wa chini kwa chini Abu Bakr al-Baghdadi, kuwa Khalifa, cheo cha kihistoria cha mtawala wa jamii ya Kiislamu.

Khalifa wa taifa la Kiislamu Abu Bakr al-BaghdadiPicha: Reuters/Rewards For Justice

Mkaazi mmoja wa Baghdad amesema kuwa wanapinga kuundwa kwa taifa la Kiislamu.

"Tunapinga kuundwa kwa taifa la Kiislamu linaloongozwa na Abu Bakr al-Baghdadi kwa kuwa linaunga mkono ugaidi. Sio taifa la Kiislamu, ni taifa la kigaidi."

Mapambano yake nchini Iraq yanaungwa mkono na makundi mengine ya Wasunni wenye silaha ambayo yanakerwa na kile wanachokiona kuwa ni ukandamizaji chini ya utawala wa Maliki.

Siku za Maliki madarakani zinahesabika

Bunge jipya lilikutana kwa mara ya kwanza tangu lilipochaguliwa mwezi Aprili, wakati matokeo ya awali yalionesha kuwa Maliki anaweza kirahisi kuthibitishwa madarakani kwa kipindi kingine cha tatu.

Lakini wakati wabunge wanakaa chini baada tu ya kuporomoka kwa ghafla kwa jeshi upande wa kaskazini, wanasiasa wanakabiliwa na jukumu kubwa la msingi la kuepusha kuvunjika kwa taifa hilo na huenda siku za waziri mkuu Maliki kubaki madarakani zikawa zinahesabika.

Marekani imetuma wanajeshi 300 zaidi nchini Iraq kusaidia kuweka usalama katika ubalozi na kuwalinda raia wa nchi hiyo na mali zao nchini Iraq.

Hatua hiyo inafikisha jumla ya wanajeshi wa Marekani walioko Iraq kwa sasa kufikia kiasi ya 750, imesema wizara ya ulinzi ya Marekani.

Picha: dapd

Wizara ya mambo ya kigeni imetangaza , wakati huo huo, kwamba inawaondoa kwa muda idadi isiyojulikana ya wafanyakazi wa ubalozi huo , kwenda katika ubalozi mdogo katika mji wa kaskazini wa Irbil na mji wa kusini wa Basra.

Hii ni pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa ubalozi kuondolewa kutoka Baghdad mapema mwezi uliopita.

Wakati huo huo kiasi ya Wairaq 2,417 wameuwawa na wengine 2,287 wamejeruhiwa , katika matukio ya ghasia na ugaidi, nchini Iraq mwezi wa Juni, umesema Umoja wa Mataifa katika taarifa leo.

Mwandishi:Sekione Kitojo

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW