1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha polisi ya Umoja wa Mataifa chaunda kikosi kipya cha polisi nchini Liberia.

Josephat Charo4 Agosti 2004

Tangu Umoja wa Mataifa kuanza mpango wake wa kuwapokonya silaha waasi nchini Liberia mwezi wa Disemba mwaka jana, jambo linalopewa kipao mbele kwa sasa ni harakati ngumu na zenye uchungu mwingi zinazotumiwa kuwasaidia waasi kuishi maisha ya kawaida katika jamii.

Mji mkuu wa Liberia, Monrovia.
Mji mkuu wa Liberia, Monrovia.Picha: AP

Mpango mwingine unaokaribia kutekelezwa ni kuleta mabadiliko katika polisi ya Liberia inayolaumiwa sana kwa ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Miaka kumi na nne ya mapigano ilisababisha polisi kutumika kama kifaa cha kutekeleza malengo ya kisiasa.

Mjumbe maalumu wa Koffi Annan nchini Liberia bwana Jacques Klein amesema watu hawakupata huduma wala msaada wa aina yoyote badala yake waliteswa na kuumizwa. Polisi iligeuka kuwa chombo cha kueneza hofu kwa wananchi badala ya kuwalinda na kuwahudumia.

Huku uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu ukikaribia, Umoja wa Mataifa umeanza kuunda kikosi cha polisi kitakachoheshimu demokrasia, haki za binadamu na kufanya kazi kwa bidii pasipo upendeleo.

Kamishna wa polisi wa kikosi cha umoja wa mataifa nchini Liberia (UNMIL) Mark Kroecker amesema wanaunda kikosi kitakachokabidhiwa mikononi mwa raia. Alisema kwamba hakukuwa na maongozi ya sheria mwaka mmoja uluiopita lakini ujumbe huo wa umoja wa mataifa bado unajitahidi kuunda na kubadilisha polisi ya Liberia.

UNMIL ina maafisa elfu moja na sabini nchini Liberia kutoka mataifa tofauiti. Maafisa hawa wako katika vituo 26 mjini Monrovia na wengine katika vituo vingine 23 nje ya mji huo. Kazi yao kubwa ni kutoa mawaidha, kusimamia na kujenga uwezo wa polisi ya Liberia ambayo mara kwa mara hufanya kazi pamoja na vikosi vya Umoja wa Mataifa.

Viongozi wa Umoja wa Mataifa wanatumai kutoa mafunzo kwa maafisa elfu 2 wa polisi kabla uchaguzi mkuu. Kufikia sasa maafisa 646 wamehitimu katika mafunzo yanayowawezesha kuchukua wadhifa wa juu katika kazi yao.

Kundi lengine la maafisa 150 na watu ambao hawajafanya kazi katika polisi wanapokea mafunzo kuhusu kazi ya polisi, kuzuia uhalifu, kudhibiti ghasia kwenye maandamano na jinsi ya kujilinda kutokana na adui.

Baada ya miezi mitatu maafisa hawa watapelekwa kufanya kazi chini ya uongozi wa walimu wao 36 kutoka mataifa tofauti. Baadaye watarudi darasani kwa mkondo wa mwisho wa masomo yao ya mwezi mmoja.

Pamoja na hayo UNMIL imefanya kampeni ya kuchagua vijana nchini kote na inachunguza maisha yao kuhakikisha kwamba wanafaa kujiunga na polisi. Watatakiwa kuwa na elimu ya shule ya upili na wawe hawajajihusisha na maovu ya ufisadi au ukiukaji wa haki za binadamu. Kikosi hiki kipya kitajumulisha watu kutoka makabila yote 16 nchini humo na kupewa mavazi mapya ya polisi.

Juhudi za umoja wa mataifa kuhusu polisi ya Liberia ni moja kati ya mambo yaliyokubaliwa katika mkataba kati ya serikali na waasi uliotiwa saini mwezi Agosti mwaka jana. Mkataba huo mbali na kukubali kuundwa kwa serikali itakayogawa mamlaka ulitoa uwezo kwa Umoja wa Mataifa kubadilisha na kuunda upya vyombo vya usalama nchini Liberia.

Mabadiliko haya kwenye polisi yamewafurahisha raia wengi wa Liberia. Henry Jones mwanafunzi wa chuo kikuu amesema maafisa wa polisi wamekuwa katili katika maongozi ya serikali za awali. Jambo hili limeipa sifa mbaya polisi na hivyo basi itabidi jitihada zifanywe ili kujenga uhusiano mwema na raia.

Kamishna wa zamani wa polisi Brownie Samukai anaamini kuwa ukosefu wa mageuzi katika polisi ulichangia kuanza tena kwa vita baada ya uchaguzi wa 1997. Amesema UNMIL imeanza mpango utakaofanya polisi iweze kutegemewa, kuheshimiwa na hata kuweza kuhudumia jamii.

Kroecker hajatangaza gharama za mabadiliko yanayofanywa. Inaonekana kuna udhamini kutoka kwa wahisani walioahidi kutoa michango yao katika mkutano wa kitaifa wa mwezi Februari mwaka jana kuhusu kuijenga upya Liberia. Hata hivyo mkurugenzi wa polisi nchini humo Clarence Massaquoi amesema bado polisi inakabiliwa na matatizo katika kutekeleza shughuli zao.

Massaquoi ameiomba serikali kushughulikia mahitaji ya polisi badala ya kutegemea jamii ya kimataifa kwa msaada. Kwa sasa maafisa wa polisi wana magari matatu pekee wanayotumia kulinda usalama na hawana tochi na mahitaji mengine.

Kroecker aliyestaafu kutoka kwa polisi ya Marekani amefanya kazi kama afisa wa polisi ya Umoja wa Mataifa katika Marekani Kusini na Marekani ya Kati. Anasema hajaona polisi isiyo na vifaa vya kufanyia kazi kama polisi ya Liberia.

Hivi karibuni Liberia imepiga hatua kubwa katika kuheshimu haki za binadamu. Hata hivyo bado kuna ukosefu mkubwa wa kazi na inahofiwa kwamba jambo hili huenda likazusha tena mapigano nchini humo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW