1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MINUSMA yaondoka mapema Ber kutokana na usalama duni

14 Agosti 2023

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, umesema Jumpili kuwa umeharakisha uondokaji kutoka kambi ya kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na hali ya usalama inayozidi kudorora.

Mali | MINUSMA Mission der Vereinten Nationen
Picha: Nicolas Remene/Le Pictorium/MAXPPP/dpa/picture alliance

Katika muda wa siku chache zilizopita, muungano wa waasi unaoongozwa na wapiganaji wa kabila la Tuareg, unaoitwa Uratibu wa mavuguvugu ya Azawad, CMA, umevituhumu vikosi vya jeshi la Mali na wapiganaji wa kundi la Urusi la Wagner, kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kuvishambulia vikosi vyake vilivoko mjini Ber. 

Jeshi la Mali halijajibu tuhuma hizo, lakini siku ya Jumamosi lilisema wanajeshi wake sita walioko Ber waliuawa wakati wakizima jaribio la uvamizi na makundi ya magaidi wasiojulikana. Na Jumapili jioni likatoa taarifa kwamba limechukuwa udhibiti wa kambi ya Ber baada ya matukio kadhaa yaliyovuruga usafiri wa vikosi vyake.

Soma pia: Kuondoka kwa kikosi cha MINUSMA nchini Mali na athari zake

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, MINUSMA ulisema katika taarifa kwamba umeharakisha uondokaji wake mjini Ber kutokana na hali ya usalama inayozidi kudorora, na kuzisihi pande zote husika kujizuwia na hatua zozote zinazoweza kuongeza ugumu katika operesheni zao, bila hata hivyo kuwataja waliohusika.

Askari polisi wa MINUSMA akitoa ulinzi katika mji wa Timbukutu, Juni 27, 2022. MINSUMA ilikuwa na jumla ya wanajeshi 11,600 na askari polisi 1,500.Picha: Nicolas Remene/Le Pictorium/MAXPPP/dpa/picture alliance

CMA yaishtumu serikali ya kijeshi kutaka kuwapoka maeneo yao

Makabiliano hayo yanafuatia madai ya kushtukiza ya Mali mnamo mwezi Juni, kwa MINUSMA kuhitimisha ujumbe wake wa muongo mzima, na kuibua wasiwasi kwamba kuondoka kwake huenda kukazidisha ugumu katika uetekelezaji wa makubaliano ya amani ya 2015 na waasi wa Tuareg na kudhoofisha juhudi za kudhibiti uasi wa makundi ya Kiislamu.

Soma pia: Ujerumani yatoa masharti kwa wanajeshi wake kubaki Mali hadi 2024

Idadi ya wanajeshi wanaohusika au ufafanuzi kuhusu tarehe ya mwanzo ya uondokaji havikutajwa, lakini katika ujumbe uliochapishwa Jumapili jioni, kikosi hicho kilisema "Msafara wa MINUSMA ulioondoka Ber ulishambuliwa mara mbili," na kuongeza kuwa walinda amani watatu waliojeruhiwa walihamishiwa mjini Timbuktu kwa ajili ya matibabu.

Ujerumani kuondoa wanajeshi wake Mali kunamaanisha nini ?

02:02

This browser does not support the video element.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani yanaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria ya kimataifa.

Ujumbe wa MINISUMA, uliokuwa na wanajeshi 11,600 na maafisa wa polisi 1,500 nchini Mali, ulianza mwaka 2013 baada ya uasi wa wanaotaka kujitenga na wapiganaji wa jihadi kuzuka kaskazini mwa Mali mwaka uliotangulia. Kujiondoa kwake kutoka kote Mali kumezidisha mzozo kati ya utawala wa kijeshi na waasi wa zamani wa vuguvugu la CMA.

Soma pia: Marekani yataka wanajeshi MONUSCO waondoke baada ya uchaguzi

CMA ilisema siku ya Jumamosi kwamba jeshi la Mali lilikuwa limedhamiria kukalia maeneo ya MINUSMA kwa gharama yoyote ile, ikiwemo maeneo yalio chini ya udhibiti wa CMA, katika ukiukaji wa makubaliano ya amani ya 2015.

Vyanzo: AFP, RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW