1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kilimo cha biashara huzidisha madhara ya ukame

26 Julai 2011

Mashambulio yaliyosababisha umwagaji mkubwa wa damu nchini Norway na janga la njaa katika Pembe ya Afrika ni mada zinazoendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani.

Basi tunaanzia Afrika Mashariki. Gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG linasema:

"Sio mamilioni bali ni mabilioni yanayohitajiwa kuhakikisha kuwa watu wa eneo la Afrika Mashariki daima, wataweza kuishi kama vile binadamu wanavyostahili. Misaada inayotolewa baada ya kila miaka kadhaa, haitowasaidia Wasomali hao - kinachohitajiwa ni msaada utakaowapa uwezo wa kujitegemea. Na jitahada za aina hiyo ziwe endelevu na ikihitajika zilindwe hata kijeshi kama ilivyokuwa safari moja katika miaka ya tisini."

Kwa maoni ya gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG nchi za Magharibi pia ni za kulaumiwa kwa madhara ya ukame yanayoongezeka katika baadhi ya nchi. Linaeleza hivi:

"Tangu miongo kadhaa, wakulima katika nchi zinazoendelea wamekuwa wakisumbuliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, kulima mazao ya biashara ili kupata mbegu za kuuzwa katika nchi za nje na badala yake nchi hizo ndio zilipatiwa misaada ya fedha. Kilimo cha aina hiyo, huathiri rutuba ya ardhi na mavuno hupunguka. Kilimo cha biashara huwanyima wakulima wengi, uwezo wa kujilisha wenyewe kama hapo awali. Kwa hivyo, ukame kila wakati, husababisha janga la njaa."

Mada nyingine kuu inahusika na mauaji ya nchini Norway. Gazeti la MITTELBAYERISCHE ZEITUNG linaeleza hivi:

"Anders Behring Breivik hajadondoka kutoka mbinguni. Mshambuliaji huyo ni mtu alieshawishiwa na itikadi kali. Yeye, sio Mkristo wa itikadli kali tu. Si mfuasi wa sera kali za mrengo wa kulia pekee. Kijana huyo, ni Mkristo wa itikadi kali na pia mfuasi wa sera kali za mrengo wa kulia. Na akili zake ni timamu. Ukatili alioufanya, unatia wasiwasi. Baada ya mauaji hayo, wala hakuonyesha hisia na hakujaribu kujiua alipokamatwa. Kwani anaamini kuwa yeye hana hatia na anaweza kuishi. Kwa maoni yake, alichokifanya ni kutekeleza wajibu wake."

Gazeti la RHEIN-ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linauliza:

"Je, jamii huru inalazimika kuvumilia mawazo yanayoweza kusababisha vifo? Kwa sehemu fulani ndio. Uhuru wa kujieleza unaodhaminiwa kisheria, umevuka mipaka yote kwa sababu ya mtandao wa internet. Mtanadao huo ni kama nyoka mwenye vichwa tisa. Tovuti moja ikifungwa, basi si chini ya mbili zingine zitafunguliwa. Mara nyingine ni kutoka nje ya nchi. Kwa hivyo, ni vigumu sana kuchuja fikra za chuki zinazoenezwa kwa njia ya mtandao. Anauesifu mtandao wa internet kama chombo cha maarifa, mawazo na cha kubadilishana habari, basi huyo hana budi pia kuukubali upande mwingine usiovutia."

Mwandishi:Martin,Prema

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW