1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kim ailaumu Marekani kwa mvutano wa eneo la Rasi ya Korea

29 Agosti 2023

Marekani, Korea Kusini na Japan zimeanza mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika eneo la bahari la Rasi ya Korea

Kim Jong Un amedai kuwa utulivu katika rasi ya Korea unahatarishwa kutumbukia kwenye vita vya nyuklia akitoa mfano wa mkutano wa hivi karibuni kati ya Marekani, Korea Kusini na Japan ambapo makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi
Kim Jong Un amedai kuwa utulivu katika rasi ya Korea unahatarishwa kutumbukia kwenye vita vya nyuklia akitoa mfano wa mkutano wa hivi karibuni kati ya Marekani, Korea Kusini na Japan ambapo makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiulinziPicha: KCNA/AP Photo/picture alliance

Hatua hiyo imekosolewa vikali na Korea Kaskazini, na kuishutumu Washington na washirika wake kuwa wanalifanya eneo hilo liliso na utulivu kuwa katika hatari ya vita vya nyuklia.

Jeshi la Korea Kusini limesema mataifa hayo matatu yanafanya mazoezi katika eneo la bahari la kimataifa, eneo la kusini mwa kisiwa cha Jeju, kwa lengo la kuboresha uwezo wao wa kubaini na kufuatilia maeneo lengwa pamoja na kubadilishana taarifa katika kile lilichoeleza kuwa kukabiliana na uchokozi wa Korea Kaskazini.

Kiongozi wa operesheni hiyo maalumu kutoka Marekani,aliyetajwa kwa jina la Kepten J anasema: "Mafunzo haya yanaboresha ushirikiano wetu na yanatutayarisha kufanikiwa katika vita endapo wapinzani wetu watafanya jaribio hilo. Zaidi yanalenga katika kujenga ujuzi wa viongozi wetu katika kila hatua. Wao ni rasilimali yetu muhimu zaidi. Muungano wetu madhubuti umeunganishwa katika kila ngazi, kuanzia  kimkakati hadi kimbinu. Tumejitayarisha kwa kila hali baharini, angani, au hata nchi kavu.”

"Kuna hatari ya vita vya nyuklia katika Rasi ya Korea."

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: KCNA/AP Photo/picture alliance

Mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika wakati kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akitoa agizo kali la kufanyiwa maboresho ya kisasa ya silaha na vifaa vya majeshi yake ya majini huku akikosoa uwepo wa kimkakati wa Marekani katika eneo hilo.

Katika hotuba ya kuadhimisha siku ya  Jeshi la Wanamaji, Kim amenukuliwa akisema "wakuu wa genge la  Marekani, Japan na Korea Kusini walitangaza luteka za mara kwa mara za pamoja za kijeshi, kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA, akimaanisha mkutano wao wa Agosti 18 wa  huko Camp David, Maryland.

Kim amesema eneo la bahari la Rasi ya Korea limegeuzwa kuwa sehemu kubwa zaidi duniani ya kupelekwa kwa vifaa vya kivita, na kulifanya eneo hilo kutokuwa na utulivu huku likigubikwa na hatari ya vita vya nyukilia.

Juhudi za kukabilina na nguvu za China na vitisho vya Korea Kaskazini

Katika mkutano wao wa kwanza wa aina yake kati ya viongozi wa Marekani, Korea Kusini na Japan, kulifikiwa makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi, pale walipokuwa wakizungumzia kile kilechoonekana kukabiliana na nguvu zinazoongezeka za China na vitisho vya silaha za nyuklia vya Korea Kaskazini.

Soma zaidi:Kim Jong Un aagiza makampuni kuongeza utengenezaji wa silaha

Wiki iliyopita Korea Kusini na Marekani zilianza kile zilichokiita "Ngao ya Uhuru ya Ulchi" mazoezi ya kijeshi ya msimu wa kiangazi ambayo yameundwa katika namna mahususi ya kuimarisha nguvu ya pamoja ya kukabiliana na vitisho vya nyuklia na makombora vya Korea Kaskazini. Lakini kwa upande wake serikali ya Pyongyang kwa muda mrefu imeshutumu kuwa mazoezi hayo ni maandalizi ya mazoezi ya vita.

Chanzo: RTR