Kim: Haturudi nyuma katika suala la nyuklia
24 Machi 2026
Kim ameyasema hayo katika hotuba yake mbele ya bunge alipokuwa akiwasilisha vipau mbele vya sera za taifa hilo.
Kim amesema Korea Kaskazini haiwezi kurudi nyuma katika hadhi yake kama taifa lenye zana za nyuklia na kutanua uwezo huo ni muhimu kwa usalama wa taifa, uthabiti wa kikanda na ustawi wa kiuchumi.
Amekanusha kuwa suala la kuachana na silaha za nyuklia haliwezikubadilishwa na manufaa ya kiuchumi au hakikisho la usalama, akisema Korea Kaskazini tayari imethibitisha kuwa na nguvu za nyuklia na kufanya juhudi za kupata maendeleo ndiyo mkakati sahihi.
Jaribio lolote litajibiwa vikali
Licha ya taifa hilo kuwekewa vikwazo na kutengwa kidiplomasia kwa miaka, rafiki huyo wa China anakadiriwa kuwa na dazeni kadhaa za vichwa vya makombora ya nyuklia na malighafi ya kutengeneza zana nyingi zaidi. Korea Kaskazini pia imekuwa ikizindua mifumo hatari ya kurusha makombora na makombora mapya ya kutoka bara moja hadi jengine yanayoweza kurushwa bila onyo.
Kim Jong Un vilevile alikuwa na kauli kali kwa jirani yake wa Kusini, Korea Kusini akisema jaribio lolote litakalofanywa na taifa hilo la kuuingilia uhuru wake litajibiwa vikali.
Korea Kusini kwa upande wake imetoa jawabu kwa kusema kauli za Kim "si nzuri kwa amani" ikiongeza kuwa ni mazungumzo na ushirikiano tu yanayoweza kuhakikisha usalama na ustawi katika rasi ya Korea.
Kim vile vile ameliambia bunge la nchi hiyo kuwa Marekani inafanya kile alichokiita "ugaidi wa kitaifa" akizungumzia mashambulizi inayoyafanya dhidi ya Iran.
Raia kutegemea mgao wa chakula cha serikali
Marekani na Israel zimesema kuwa mashambulizi yake nchini Iran ni ya kuizuia Jamhuri hiyo ya Kiislamu kutounda silaha za nyuklia, ila Korea Kaskazini iko hatua nyingi mbele katika suala hilo.
Sambamba na sera za kiusalama, Kim amewasilisha pia vipau mbele vya kiuchumi katika hotuba yake hiyo kwa bunge akitoa wito kwa maafisa wa nchi hiyo kutekeleza mpango mpya wa miaka mitano wa maendeleo, uliojikita katika kuvifanya viwanda nchini humo kuwa vya kisasa, kuongeza uzalishaji wa nguvu za umeme na mkaa, kuongeza uzalishaji wa chakula na kutanua ujenzi wa nyumba za makaazi kote nchini humo.
Korea Kaskazini ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani kutokana na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa, huku kukiwa na mapungufu makubwa yaliyowapelekea raia wake kutegemea mgao wa chakula wa serikali.
Vyanzo: AFP/Reuters