1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Un aitisha kikao cha dharura

30 Desemba 2019

Wakati muda wa mwisho wa mazungumzo na Marekani juu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini ukiwadia, kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong Un, ameitisha mkutano wa dharura wa maafisa wakuu wa kijeshi na kidiplomasia.

Nordkorea Kim Jong Un
Picha: Reuters/KCNA

Kwenye taarifa yake ya leo, shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limesema kiongozi huyo alizungumza kwenye mkutano maalum wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea, akielezea matatizo yanayoikumba sekta ya viwanda na wakati huo huo akiwapangia majukumu wasaidizi wake kurekebisha matatizo hayo.

Kim alitaka pawepo na matayarisho ya haraka ya kisera juu ya masuala ya kiusalama, silaha na kile alichosema kuwa ni ulinzi wa uhuru wa Korea Kaskazini.

Kauli hizi zimetafsiriwa na mahasimu wake wa Korea Kusini na Marekani kwamba ni dalili zisizo njema kuelekea muda wa mwisho aliokuwa ameuweka wa tarehe 31 Disemba 2019, ambapo alitaka utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani uwe umeshalainisha msimamo wake kwenye mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Kuna wasiwasi kwamba huenda kwenye hotuba yake ya mkesha wa mwaka mpya, Kim akaamuru kusitishwa kwa mazungumzo hayo na badala yake kurejea kwenye majaribio ya makombora ya masafa marefu, ambayo aliyasitisha tangu mwaka 2017.

Korea Kaskazini inaitaka Marekani kuacha kuiwekea vikwazo mara moja, ikiwa inataka kuyaokowa mazugumzo  hayo.

Korea Kusini ipo kwenye tahadhari

Kwenye mkutano wa Juni 2019 kati ya Kim Jong Un na Donald Trump, viongozi hao waliahidi kuendelea na mazungumzo baadaye.Picha: AFP/Getty Images/B. Smialowski

Ingawa shirika la habari la KCNA halikusema endapo kwenye hotuba yake, Kim aliitaja moja kwa moja Marekani wala ikiwa maamuzi rasmi yalifikiwa na kikao hicho cha dharura, lakini msemaji wa Korea Kusini wa wizara inayohusika na kuungana tena kwa Korea hizo, Lee Sang-min, alisema nchi yake inafuatilia kwa makini mkutano huo wa chama tawala. 

Cheong Seong Chang, mchambuzi wa ngazi za juu kwenye Taasisi ya Sejong nchini Korea Kusini, amesema hii ni mara ya kwanza chini ya utawala wa Kim kwa mkutano kama huo wa dharura kuitishwa na kuendelea kwa zaidi ya siku moja. 

"Inaonekana Kim anahitaji kwa haraka sana kufanya mabadiliko makubwa mbele ya shinikizo na vikwazo vinavyoendelea vya Marekani, hasa kutokana na kushuka kwa usafirishaji wa bidhaa za nje kunakoukwamisha uchumi wa Korea Kaskazini," alisema mchambuzi huyo. 

Kim ameshakutana na Rais Trump mara tatu ndani ya kipindi cha miaka miwili, lakini juhudi za kidiplomasia zimeshindwa hadi sasa kuishawishi Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia na makombora ya masafa marefu. 

Kwenye mkutano wao wa mwisho mnamo mwezi Juni, pande hizo mbili zilikubaliana kurejea kwenye mazungumzo tena, lakini kikao cha matayarisho cha mwezi Oktoba nchini Sweden kilivunjika, huku wajumbe wa Korea Kaskazini wakiwalaumu wenzao wa Marekani kwa kushikilia msimamo "mkongwe na kuwa na kiburi."