1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kaskazini

Kim Jong Un akutana na wajumbe kutoka Urusi na China

27 Julai 2023

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amekutana na waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu pamoja na wajumbe kutoka China katika wakati nchi hiyo ikiadhimisha miaka 70 tangu kumalizika vita vya Korea.

Nordkorea, Pjöngjang | Kim Jong-un, Sergej Schoigu und Li Hongzhong bei 70. Jahrestag des Waffenstillstands
Picha: AP Photo/picture alliance

Kim na Shoigu wamejadili masuala ya kijeshi na mazingira ya usalama wa kikanda. Hata hivyo, haikuwekwa wazi masuala ya kijeshi yaliyojadiliwa katika mkutano wa viongozi hao wawili.

Shoigu ambaye ni mjumbe wa Rais wa Urusi, amekutana na kiongozi wa Korea Kaskazini na kumkabidhi Kim barua "nzuri" iliyotiwa saini na Rais Vladimir Putin.

Urusi, mshirika wa kihistoria wa Korea Kaskazini,  ni mojawapo ya mataifa machache ambayo Pyongyang imedumisha uhusiano wa kirafiki.

Korea Kaskazini ambayo imekuwa ikiongozwa kidikteta na familia ya Kim tangu miaka ya 1950, kwa kiasi kikubwa imetengwa kimataifa kwa sababu ya mpango wake wa silaha za nyuklia, lakini imeendeleza mawasiliano na nchi mbili wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni China na Urusi.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un (Kulia) akiwa na Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu: Pyongyang,26.07.2023Picha: KCNA/REUTERS

Korea Kaskazini imekuwa ikiiunga mkono Urusi katika vita vyake na Ukraine ikisema nchi za Magharibi zinazoongozwa na Marekani, ndizo zilizoipelekea Urusi kuchukua hatua za kulinda maslahi yake ya kiusalama.

Kabla ya safari hiyo, wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema ziara ya siku tatu huko Pyongyang itaimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na Korea Kaskazini, na kwamba ni hatua muhimu ya kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

Marekani inaishuku Korea Kaskazini  kuiunga mkono Urusi kwa kuipatia silaha inazotumia katika uvamizi wake dhidi ya Ukraine. Kikundi cha mamluki cha Wagner, ambacho kinashirikiana na vikosi vya Moscow pia inasemekana kilipewa vifaa na silaha na utawala wa Pyongyang. Hata hivyo Korea Kaskazini imekuwa ikikanusha mara zote kutoa silaha na risasi kwa Urusi.

Kim akutana pia na Ujumbe kutoka China

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un (Kushoto) akisalimiana na Mjumbe wa chama cha Kikomunisti cha China Li Hongzhong mjini Pyongyang, 27.07.2023Picha: KCNA/REUTERS

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amekutana pia na ujumbe wa China ulioongozwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti. Kim amempokea siku ya Alhamisi Li Haongzhong mjini Pyongyang, ambapo alimkabidhi pia barua rasmi ya Rais wa China, Xi Jinping.

Soma pia: Kim Jong Un aapa kuendelea kuimarisha uwezo wa nyuklia

Korea Kaskazini inaadhimisha Alhamisi hii ya Julai 27,2023 miaka 70 ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwaka 1953, ambayo yalimaliza uhasama kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini na yanayoadhimishwa mjini Pyongyang kama Siku ya Ushindi.

Mkataba huo wa kusitisha mapigano uliigawa Korea na kuwa mataifa mawili. Kulingana na makadirio, Wakorea wapatao milioni 2 hadi milioni 4 waliuawa katika vita hivyo vya mwaka 1950-1953.