Kim Jong Un ameiomba msamaha Korea ya Kusini
25 Septemba 2020Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un ameomba radhi leo baada ya wanajeshi wa nchi yake kumpiga risasi na kumuua afisa wa wizara kutoka Korea kusini karibu na mpaka wa baharini wa nchi hizo mbili.
Shirika la habari la Korea kusini limeripoti kuwa katika ujumbe wake Kim Jong Un, amesema amesikitishwa mno kwamba amemvunja moyo rais wa Korea kusini Moon Jae In, likinukuu taarifa kutoka ofisi ya rais.
Suh Hoon,mshauri wa baraza la usalama wa Taifa ,Korea ya Kusini alisoma barua kutoka kwa chama tawala cha Korea ya Kaskazini inayosema serikali ya Pyong Yang imekiri kufyetuwa risasi zaidi ya kumi kwa mtu huyo aliyeingia kinyume cha sheria kwenye eneo la maji yake na ambaye alikataa kujitambulisha.
''Rais Kim Jong Un ametuambia katika ujumbe wake kwamba amesikitishwa na tukio hilo na kusema pahali pa kusaidia raia wa Korea ya Kusini wanaotaabika na tishio la ugonjwa wa Corona, kumetokea kwenye eneo la maji yetu tukio lisilotarajiwa na la aibu, ambalo limewasikitisha rais Moon na raia wake wa Korea ya Kusini.'',alisema Hoon.
Barua hiyo inasema walinzi wa mipaka wa Korea ya Kaskazini walimuua kufuatia amri walizopewa.
Ijumaa serikali ya PyongYang haikuthibitisha uwepo wa barua hiyo na vyombo vya habari vya Korea ya Kaskazini havikuripoti kuhusu tukio hilo.
Matumaini ya maridhiano baina ya Kim na Moon
Wadadisi wanaelezea kwamba kufuatia ujumbe huo, Korea ya Kaskazini inajaribu kutumtuliza jirani wake wa Kusini,ambako mauwaji hayo ya kwanza kufanywa na jeshi la Korea Kaskazini mnamo kipindi cha miaka 10,yalizusha mhemuko.
Ahn Chan-Il, aliyetoroka Korea ya Kaskazini na ambaye amefanya utafiti mjini Seoul, amesema kwamba ni nadra sana kiongozi wa Korea ya Kaskazini kuomba msamaha kwa Korea ya Kusini.
Leif Eric Easley, Profesa kwenye chuo kikuu cha Ewha, mjini Seoul amesema Kim Jong Un kuomba msahama kunapunguza athari za kuweko na makabiliano baina ya nchi mbili hizo na kuwepo na matumaini ya maridhiano na rais Moon.
Wanajeshi walimpiga risasi mtu huyo siku ya Jumanne, kwa sababu walifikiri kuwa ni mvamizi. Wizara ya ulinzi ya Korea kusini ilisema hapo kabla kuwa afisa huyo mwenye umri wa miaka 47, na mfanyakazi wa wizara inayoshughulikia masuala ya bahari na uvuvi ya Korea kusini, alitoweka kutoka katika boti wakati akiwa katika ujumbe wa ukaguzi kiasi ya kilometa 10 kusini mwa mpaka wa baharini na Korea kaskazini.
Baadaye mwili wa afisa huyo uliosalia kwenye maji,aminika kuchomwa moto na wanajeshi wa Korea ya Kaskazini kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona.