1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Un asitisha hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kusini

24 Juni 2020

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amefutilia mbali mipango ya hatua ya kijeshi dhidi ya jirani yake Korea Kusini. Hatua hiyo inachukuliwa kuwa ni uamuzi wa ghafla wa kupunguza mivutano.

Spannungen zwischen Nordkorea und Südkorea
Picha: picture-alliance/dpa/AP/Ahn Young-Joon

Katika wiki za karibuni serikali ya mjini Pyongyang ilitowa kauli kali za kuilaani Korea Kusini kuhusu vipeperushi vilivyokuwa na ujumbe dhidi ya nchi hiyo ya Korea Kaskazini vikitumwa kupitia mpakani kwa kutumia chupa au maputo na watu  walioihama nchi hiyo na kukimbilia Kusini.

Wiki iliyopita Korea Kaskazini iliishambulia ofisi ya ushirikiano iliyoko upande wa mpaka wake ofisi ambayo ikionekana kama ishara ya mjongeleano wa Korea hizo mbili,huku jeshi la nchi hiyo likisema litachukua hatua kadhaa dhidi ya jirani yake Kusini.

Hatua zilizolengwa kuchukuliwa na jeshi hilo ni pamoja na kuingia tena kwenye maeneo ya kaskazini ambayo ilijiondowa kama sehemu ya juhudi za mjongeleano wa Korea mbili,kadhalika kurudisha upya vituo vyake vya ulinzi katika eneo lisilotakiwa shughuli za kijeshi ambalo liko mpakani sambamba na kuongeza harakati za mazoezi ya kijeshi.

Vipeperushi vinavyodaiwa kurushwa upande wa Korea KaskaziniPicha: Reuters/Kim Hong-Ji

Lakini katika kile kinachoonekana kama hatua ya kubadilisha mkondo,shirika rasmi la habari la serikali ya Korea Kaskazini Jumanne likatangaza kwamba kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un aliongoza mkutano wa kamati kuu ya jeshi ambapo alifutilia mbali hatua za kijeshi zilizokuwa zimepangwa dhidi ya Korea Kusini.

Na kama haitoshi shirika la habari la Kusini Yonhap limeripoti bila ya kutaja vyanzo vyake kwamba Korea Kaskazini pia imeondowa vipaza sauti Jumatano kutoka maeneo ya mpaka,ambavyo vilikuwa vimeanza kuwekwa siku mbili tu zilizopita kwa lengo la kutangaza propaganda za kuipinga Korea Kusini.

Juu ya hilo vituo vya propaganda vya serikali mjini Pyongyang vimefutilia mbali ripoti ambazo zimekuwa zikiikosoa Korea Kusini kwa mujibu wa wizara ya Korea Kusini inayohusika na masuala ya kuziunganisha Korea mbili,wizara ambayo inashughulikia suala la mahusiano na nchi hiyo ya Korea Kaskazini.

Kimsingi hatua hizi za Korea Kaskazini sio za kawaida na zimekuja baada ya wachambuzi kusema kwamba nchi hiyo inataka kuutengeza mgogoro katika rasi hiyo katika juhudi za kutaka kusikilizwa. Hata hivyo wizara ya Korea Kusini inayohusika na suala la mahusiano na nchi hiyo jirani yake wa Kaskazini imesema inafuatiliwa kwa karibu na kwa makini huku ikitathmini ripoti zilizotangazwa na shirika rasmi la habari la KCNA ambalo lilisema kwamba mkutano huo wa Kim Jong Un ulifanyika kwa njia ya Vidio,kitu ambacho kwa mujibu wa wizara hiyo ya Korea Kusini inakiona ni kipya.

Kim Yo Jong dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong unPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Sung-Doo

Ikumbukwe kwamba Korea Kusini iliikosoa vikali Kaskazini na kukitaja kitendo chake cha kuishambulia ofisi ya ushirikiano pamoja na kauli chafu za kumshutumu rais Moon Jae In zilizotolewa na dada wa Kim Jong Un,Kim Yo Yong ni mambo hayatoendelea kuvumiliwa pamoja na vitendo na kauli zisizokuwa na msingi. Uhusiano baina ya majirani hao wawili ulizidi kutumbukia kwenye hali ya mkwamo kufuatia kuporomoka kwa mkutano wa kilele mjini Hanoi,Vietnam kati ya Kim Jong Un na rais wa Marekani Donald Trump mwanzoni kabisa mwa mwaka jana.

Nchi hiyo masikini kabisa ya Korea Kaskazini inakabiliwa na vikwazo chungu nzima vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na miradi yake ya silaha ambayo imepigwa marufuku.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW