1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Un kukutana na Vladimir Putin

24 Aprili 2019

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amewasili mjini Vladivostok, kwa mkutano wake wa kwanza na rais Vladimir Putin, akitafuta uungwaji mkono katika mkwamo wa kujadili mpango wake wa nyuklia na Marekani.

Kombibild - Vladimir Putin und Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Photo//D. Lovetsky/E. Vucci

Mazungumzo hayo yaliyopangwa kwa usiri mkubwa na kutangazwa hadharani katika dakika za mwisho, yatakuwa wa kwanza ya ana kwa ana kati ya Kim na kiongozi mwengine wa taifa, tangu kuvunika kwa mazungumzo kati yake na rais wa Marekani Donald Trump yaliyofanyika mjini Hanoi mwezi Februari.

Treni iliyombeba Kim iliwasili mchana wa leo katika kituo cha treni cha Tsarist-era katika mji  wa Vladivostok.

Rais Kim Jong Un akilakiwa kwa gwaride la heshima baada ya kuwasili UrusiPicha: Reuters/S. Zhumatov

Rais huyo wa Korea Kaskazini alilakiwa kwa gwaride la heshima huku kukiwa na wanawake waliokuwa wamebeba mikate na chumvi wakimpokea na kumsalimu kama sehemu ya salamu za kitamaduni.

Baadaye alilakiwa pia na gavana wa eneo la Primorye Oleg Kozhemyako, Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Igor Morgulov na balozi wa Urusi nchini Korea Kaskazini Alexander Matsegora.

Akizungumza na televisheni ya kitaifa baada ya kuwasili kwake Kim Jong Un alisema anatumai ziara yake itakuwa ya mafanikio makubwa.

Urusi inanuia kuionyesha dunia inabakia kuwa muhimu licha ya vikwazo ilivyoekewa

Kim ameongeza kuwa anatumai mwishoni mwa ziara hiyo, atafanikiwa kuwa na mazungumzo muhimu ya kutatua mizozo katika rasi ya Korea na maendeleo ya mahusiano ya nchi hizo mbili. Bendera za Urusi na Korea Kaskazini zilionekana zikipepea katika milingoti siku ya Jumanne katika kisiwa cha Russky mjini Vladivostok, ambako Putin na Kim wanatarajiwa kukutana hapo kesho.

Mazungumzo kati ya viongozi hao yanafanyika baada ya mialiko ya mara kwa mara kutoka kwa Putin tangu Kim alipoanza safari yake ya kutafuta uungwaji mkono juu ya mpango wa nyuklia wa nchi yake.

Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: picture alliance / Mikhail Metzel/TASS/dpa

Tangu mwezi Machi mwaka 2018 Kim amekuwa na mikutano minne na rais wa China Xi Jinping, mikutano mitatu na rais wa Korea Kusini Moon Jae In, mikutano miwili na rais wa Marekani Donald Trump na mmoja na rais wa Vietnam Nguyen Phu Trong.

Lakini wachambuzi wanasema Kim kwa sasa anatafuta uungwaji mkono mkubwa wa Kimataifa baada ya kukwaruzana na Marekani huku  Urusi nayo ikiwa makini kutanua ushawishi wake duniani.

Kwa Putin mkutano huu unatoa nafasi pia ya kuionyesha dunia kuwa nchi yake inabakia kuwa muhimu licha ya vikwazo ilivyoekewa kufuatia madai ya kuingilia Ukraine na kuuingilia uchaguzi wa Marekani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW