1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Idai chaupiga mji wa Beira, Msumbiji

Daniel Gakuba
15 Machi 2019

Kimbunga kikali kimeupiga mji wa Beira kwenye pwani ya Msumbiji, kikijeruhi watu wengi na kuharibu miundombinu. Kimbunga hicho, ''Idai'' kimefuatia mafuriko katika nchi za Kusini mwa Afrika, yaliyouwa watu zaidi ya 120.

Überschwemmungen in Mosambik 2013
Picha: AFP/Getty Images/U. Mamudo

 

Kimbunga hicho kilitua mjini Beira Alhamis jioni kikiambatana na mvua kubwa na upepo unaovuma kwa kasi ya km 170 kwa saa. Picha za televisheni na zilizowekwa katika mtandao wa twitter zimeonyesha mapaa ya nyumba yakiezuliwa na upepo huo, vibao vikubwa vya matangazo ya biashara vikipeperushwa hewani, na nguzo na nyaya za umeme vikiangushwa katika mji huo wa pwani ya Msumbiji wenye wakati zaidi ya 500,000.

Baadhi ya vijiji pwani katika mkoa wa Zambezi Kaskazini mwa Msumbiji vimegeuka visiwa, vikitenganishwa na sehemu na sehemu nyingine za nchi na maji yaliyojaa sehemu za mabonde. Shirika la televisheni la Msumbiji limeripoti kuwa watu wasiopungua watano wamejeruhiwa vibaya na kimbunga Idai.

Majanga yaenea hadi Chinde

Afisa mmoja wa idara ya taifa ya kupambana na athari za majanga, Pedro Armando Alberto Virgula  amesema kimbunga Idai kimeupiga pia mji mwingine wa Chinde, na kuharibu paa za hospitali na za nyumba za watu.

Awali, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu msaada wa kibinadamu ilikuwa imetoa tahadhari, kwamba kimbunga hicho kingekuwa na kasi ya hadi km 190 kwa saa.

Kabla ya kimbunga hiki kufika nchi kavu, tayari maeneo makubwa ya Msumbiji, Malawi na Afrika Kusini yalikuwa yameathiriwa na mafuriko, ambayo yameuwa watu 126 na kuwafanya wengine wapatao milioni moja kuyakosa makaazi.

Francis Kadzokoya, afisa ahusikaye na masuala ya dharura katika wilaya ya Chikwawa Kusini mwa Malawi, amesema mafuriko hayo yamewaweka katika hali ngumu.

''Kusema kweli hali inatisha, kwa kuzingatia ukubwa wa janga lililoipiga wilaya hii, kwa sababu kaya 12,432, ambazo zina watu 52,511 zimepoteza makaazi. Idadi kama hiyo ya watu waliogeuzwa wakimbizi wa ndani ni changamoto kubwa kwa wilaya ya Chikwawa.'' Amesema Kadzokoya.

Kiwango kamili cha uharibifu hakijulikani bado

Afisa mkuu wa kitengo cha utabiri wa hali ya hewa nchini Afrika Kusini, Jan Vermeulen amesema hali jumla ya uharibifu iliyosababishwa na kimbunga Idai bado haijulikani, kwa sababu hakuna mawasiliano na sehemu zilizoathiriwa.

Hii sio mara ya kwanza Msumbiji na nchi jirani kukumbwa na kimbunga. Mwezi Februari mwaka 2000 kimbunga Eline kiliuwa watu 350 na kuwaacha wengine 650,000 bila makaazi.

Maeneo yenye utajiri mkubwa wa gesi Kaskazini mwa Msumbiji yamenusurika kimbuka hiki, ambacho kimejikita katika eneo la Kusini mwa nchi.

rtre,afpe