1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Idai: Msaada waanza kufika maeneo yaliyoathirika

Daniel Gakuba
20 Machi 2019

Msaada wa kimataifa umeanza kuwasili katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi, ambazo zimeathiriwa vibaya na mafuriko yaliyoambatana na kimbunga Idai, na waliothibitika kuuawa na kimbunga hicho imefika watu 300.

Simbabwe Zyklon Idai Hilfsgüter
Shughuli za kusambaza msaada zimeanza kushika kasiPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Zoezi la kuwafikishia msaada wanaouhitaji lilianza kwa mwendo wa kujivuta kwa sababu miundombinu muhimu kama viwanjwa vya ndege imeharibika vibaya, lakini sasa limeanza kushika kasi baada ya mataifa ya kigeni kuingilia kati. Kulingana na Caroline Haga ambaye ni mfanyakazi wa shirika la Msalaba Mwekundu  nchini Msumbiji, wahisani wengi hivi sasa wamezidisha mara mbili au tatu kiwango cha msaada walichokuwa wameahidi awali.

Umoja wa Ulaya umekwishatenga dola takribani milioni 4 kwa ajili ya msaada wa dharura, Uingereza imeidhinisha dola milioni 8, na nchi jirani ya Tanzania imepeleka tani 238 za msaada wa chakula na madawa, zikibwebwa na ndege zake za kijeshi.

Walionusurika kimbunga Idai wakihamisha kidogo walichobaki nachoPicha: picture-alliance/dpa/D. Onyodi

Idadi ya watu ambao wamethibitika kuuawa na kimbunga Idai imekwishafika watu 300, hizo zikiwa takwimu za Msumbiji na Zimbabwe tu, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka mara tatu zaidi ya hiyo ya sasa. Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema watu 350,000 nchini mwake wanakabiliwa na kitisho kikubwa, na ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa ajili ya waliouawa na kimbunga Idai.

Watu waokolewa kutoka paa za nyumba

Wafanyakazi wa shughuli za uokozi wanatumia mitumbwi na helikopta kuwatafuta manusra wanaojihifadhi juu ya paa za nyumba na kwenye matawi ya miti. Shirika moja liitwalo Rescue South Africa limesema tangu Ijumaa iliyopita, limewaokoa watu 34 kwa kutumia helikopta.

Kimbunga Idai kimeharibu miji na vijijiPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Onyodi

Nchini Zimbabwe, Rais Emmerson Mnangagwa ametembelea eneo la Chimanimani lililokumbwa na mafuriko mabaya, na amesema nchi jirani zinazoizunguka Zimbabwe zinataka kutoa usaidizi.

''Nchi kama Afrika Kusini, Botswana, Namibia na Angola zimetaka kujua msaada tunaouhitaji, na tuko mbioni kuorodhesha vitu vinavyohitajika, ambavyo tunaamini wanaweza kutusaidia kuvipata.'' Amesema.

Dunia haijatambua ukubwa wa tatizo

Mashirika ya kimataifa pia yamewasili, likiwemo lile la chakula ulimwenguni WFP ambalo limeahidi kuwasaidia watu kati ya 500,000 na 600,000. Msemaji wa shirika hilo Herve Verhoosel amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, kwamba inavyoonekana dunia bado haijatambua ukubwa wa matatizo katika ukanda wa Kusini Mashariki mwa Afrika.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu msaada wa kibinadamu, OCHA tayari linasaidia kukusanya taarifa na kuzishughulikia, wakati UNICEF likisambaza vifaa muhimu kama mahema, maji safi na vifaa vya shule kwa watoto waliopoteza kila kitu.

afpe,ape