1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Irma chazidi kushika kasi

8 Septemba 2017

Kimbunga Irma kwenye maeneo ya Carrebean na Atlantiki na tetemeko la ardhi nchini Mexico ni sehemu ya uthibitisho kwamba mabadiliko ya tabia nchi ni kitisho cha kweli kwenye dunia ya sasa.

Sint Maarten Saint Martin Hurrikan Irma
Picha: Reuters/Netherlands Ministry of Defence-Gerben van Es

Dunia inaonekana kuvamiwa na majanga makubwa ya kimaumbile yakiwa yamefuatana sana kiasi cha kuwatisha watabiri ya hali ya hewa ulimwenguni. Kutoka Carrebean hadi Atlantiki, Afrika hadi Marekani, kitisho kinachotokana na mabadiliko ya tabia nchi kiko wazi, na hasara kwa maisha ya mwanaadamu ni kubwa sana.

Gavana wa jimbo la Chiapas nchini Mexico anasema watu watatu hadi sasa wamekufa kutokana na tetemeko lenye ukubwa wa 8.1 kwa vipimo vya Richter lililopiga eneo la kusini mwa taifa hilo la Amerika Kusini. Picha za televisheni zinaonesha nyumba zikitikisika na kuporomoka, huku kukiwa na tahadhari ya kutokea kwa tsunami. 
Namna tetemeko hilo la leo lilivyokuwa kubwa, limetikisa hadi sehemu zilizokuwa umbali wa kilomita 1,000 kutoka kiini chake. 

Nchini Haiti, taifa la visiwa vya Carrebean, Kimbunga Irma kimeupiga vibaya mji wa pwani wa Hispaniola, huku upepo ukivuma kwa kasi ya kilomita 295 kwa saa. Mamlaka nchini humo zimezifunga shule na kuwahamishia watu kwenye maeneo salama, kwa msaada wa wafanyakazi wa kujitolea na wanajeshi.

Kuna wasiwasi kwamba huenda Kimbunga Irma kikaleta maafa makubwa zaidi nchini Haiti, taifa ambalo tayari limeshaathiriwa vibaya na ukame, anasema mkurugenzi  mkaazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Ronald Tran Ba Huy.

Carrebean, Atlantiki Zakumbwa vibaya

Jamhuri ya Dominic, visiwa vya Turks, Caicos na Bahamas, vyote vilikutwa na zilzala hiyo hapo jana, ambacho Idara ya Kushughulikia Majanga ya Kimbunga nchini Marekani imekiweka kwenye Kigawe Namba 5. 

Viongozi wa zamani wa Marekani waungana kusaidia waathirika wa vimbunga.Picha: picture alliance/AP Photo/J. S. Applewhite

Hali ilikuwa sawa kwa visiwa vya Virgin, Saint Martin, Saba na Sint Eustasius vinavyomilikiwa na Marekani, Uholanzi na Ufaransa. Gavana wa kisiwa cha Virgin, Kenneth Mapp, anasema visiwa hivyo vinahitaji msaada wa haraka sana kutoka serikali kuu, mjini Washington, baada ya Kimbunga Irma kuviharibu vibaya visiwa vya Saint Thomas na Saint John kikitembea kwa kasi ya kilomita 241 kwa saa, kwa zaidi ya masaa manne. 

Muda huu tukiwa hewani, zilzala hiyo inaelekea katika jimbo la Florida nchini Marekani, ambako tayari serikali imechukuwa tahadhari ya kuwahamisha maelfu ya watu kutoka fukwe za eneo hilo. Gavana wa Florida, Rick Scott, amewaonya wakaazi kutokukaidi amri hiyo, licha ya kuwa hatua za uokozi zimeshatayarishwa. 

Rais Donald Trump, ambaya daima anakanusha kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi akisema na uzushi wa wanasayansi na wanaharakati wanaotaka kujipatia fedha, ameelezea wasiwasi wake juu ya Kimbunga Irma wakati kikivuka Bahari ya Caribbean kuelekea Marekani, akisema anasimama pamoja na watu wa Florida. 

Kwa uchache, watu 15 wameshakufa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kimbunga hicho kikubwa kabisa, kuwahi kutokea katika Bahari ya Atlantiki. 

Hiki ni kimbunga cha pili ndani ya wiki moja, kikitanguliwa na kile kilichopewa jina Harvey, ambacho kiliukumba mji wa Texas. Marais watano wa zamani wa Marekani - Barack Obama, Bill Clinton, George Bush Mkubwa na Mdogo pamoja na Jimmy Carter - wameanzisha kampeni ya pamoja kuwasaidia waathirika wa kimbunga hicho. 

Qatar, taifa dogo la Kiarabu lenye utajiri wa mafuta, limetoa dola milioni 300 kusaidia kampeni ya kuijenga upya miundombinu ya Texas.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga