1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga "Jobo" kupiga Pwani ya Tanzania na Zanzibar

Salma Mkalibala23 Aprili 2021

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imeendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wake juu ya ujio na mwenendo wa kimbunga "Jobo”kilichopo bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.

Australien Zyklon Seroja
Picha: EOSDIS via AP/picture alliance

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imeendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wake juu ya ujio na mwenendo wa kimbunga "Jobo”kilichopo bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar, ambapo Kimbunga Jobo kimendelea kuimarika na kusogea kwenda uelekeo wa maeneo ya pwani ya nchi hiyo na kutajwa kuathiri mikoa ya pwani. 

Kulingana na taarifa iliyotolewa leo mchana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa, Agness Kijazi kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam na kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya mamlaka hiyo imeeleza kuwa, hadi kufikia usiku wa kuamkia kesho aprili 24, kimbunga hiko kinatarajiwa kuwa umbali wa takriban kilomita 235 mashariki mwa kisiwa cha Mafia na baadaye mchana wake kuwa umbali wa takribani kilomita 125 mashariki mwa Mafia.

Soma zaidi: KANSAS:Kimbuga chaua watu tisa na kuusambaratisha mji

Amesema kimbunga Jobo kimeambatana na upepo mkali unaofikia kilimita 90 kwa saa, na mwelekeo wake ni katika pwani ya kilwa na Dar es salaam na hadi kufikia kesho kimbunga kitakuwa kimesogea zaidi na kasi ya upepo inatarajiwa kufikia kilimota 70 kwa saa.

April 25 upepo utafikia kasi ya kilometa 60 kwa saa, mawimbi makubwa baharini pamoja na ongezeko la mvua kwa maeneo ya ukanda wa pwani vinatarajiwa kujitokeza.

Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar ni miongoni mwa sehemu zinazotarajiwa kupata athari za kimbuga Jobo

Kimbuga Eloise kimefanya uharibifu mkubwa wa mazingira nchini MsumbijiPicha: TWITTER/@BEN_VW/REUTERS

Maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja kutokana na kimbunga Jobo ni pamoja na mikoa yote ya Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), mikoa ya Lindi na Mtwara, Dares Salaam, Tanga pamoja na kisiwa cha Unguja na pemba .

“Kwa hiyo tunatakana tu tutoe tahadhari, kwa wananchi wote katika ukanda wote wa pwani, inaamana kwamba kuanzia Mtwara, Lindi, Kisiwa cha Mafia, Dar es salaam, pamoja na Kisiwa cha Unguja na mkoa wote wa Pwani pia, waweze kuchukua tahadhari hii ya upepo mkali ambao unatarajiwa hasa kipindi hicho ambacho kimbuka sasa kitakuwa kimetua hii tarehe 25”

Hata hivyo, uwepo wa kimbunga Jobo unatarajiwa kuendelea kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini na kusababisha ongezeko la vipindi vya mvua kwa maeneo mengine yaliyo mbali na ukanda wa pwani ikiwemo ukanda wa Ziwa Victoria.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa amewataka wanachi wanaotumia bahari kuchukuwa tahadhari kwa kuwa kumejitokeza hali ya upepo mkali na mawimbi makubwa baharini na kushauriwa kusitisha shughuli zao za baharini hadi pale hali hiyo ya kimbunga inatakapopita, sambamba na kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa.

“Kunapokuwa na kimbunga kinatabia ya kuvuta mawingu kutoka magharibi kwa maana ya maeneo kutoka misitu ya Congo, tayari kuna mawingu ambayo yamejijenga katika maeneo ya Ziwa Victoria, kwa hiyo kadri kimbunga kinavyoendelea kusogea tunatarajia pia maeneo yaliyopo magharibi yataweza kupata athari kwa maana ya kuwa na vipindi hivi vya mvua kubwa” aliongeza Mkuu huyo wa Hali ya hewa Tanzania.

Kutokana na uwepo wa taarifa hizo ambazo zilianza kutolewa tangu april 21, DW imezungumza na baadhi ya wakazi wa Mikoa wa Lindi na Mtwara, na kuhoji juu ya tahadhari wanazozichukua.

“ Kwanza kabisa nimeweza kuwasiliana na familia yangu kwa sababu siishi na familia yangu, kwa hiyo nimewasiliana na familia yangu na kuiambia wachukue tahadhari kama tulivyoambiwa kesho na kesho kutwa pengine watoto wasitembee, wasitoke nyumbani ili waweze kukaa sehemu ambayo ni salama,” ameeleza Stella Kihombwo mkazi wa Lindi.

 Licha ya kutolewa kwa tahadhari lakini wanachi walio wengi hawatambui kinachoendelea juu ya kimbunga jobo.

“Sina taarifa yoyote maana tangu juzi nipo kwenye shughuli zangu, kwa hiyo sijapata taarifa yoyote kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa;” amesema Hamis Juma mkaazi wa mkoa wa Lindi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW