Kimbunga Oscar chapiga Cuba na kuzidisha matatizo ya umeme
21 Oktoba 2024Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Cuba (Insmet) imesema Kimbunga Oscar kilipiga kwenye pwani ya Cuba katika jimbo la Guantanamo, karibu na mji wa Baracoa, mashariki mwa kisiwa hicho.
Hayo yanajiri wakati serikali ya Cuba ikijitahidi kutatua tatizo la ukosefu wa umeme ambalo limedumu kwa siku tatu kutokana na hitilafu kwenye mtambo mkubwa wa umeme. Rais wa visiwa hivyo Miguel Díaz-Canel amesema watachukua hatua kali dhidi ya wale watakaovuruga hali ya utulivu wakati nchi hiyo ikiwa kwenye giza.
Soma pia: Mamilioni ya Wacuba gizani baada ya umeme kukatika nchi nzima
Kwa zaidi ya miezi mitatu raia wa Cuba wanakabiliwa na mgao wa umeme ambao umekuwa ukitatiza shughuli za kijamii na kiuchumi. Kukatika kwa umeme ni mojawapo ya vichochezi vya maandamano ya kihistoria ya Julai 11, mwaka 2021. Mnamo Septemba mwaka 2022, kimbunga Ian kilichopiga magharibi mwa Cuba kilisababisha kwa siku kadhaa matatizo ya kukatika kwa umeme.