Kimbunga Rita kuikumba tena Marekani
20 Septemba 2005Miami:
Majuma matatu baada ya kutokea kimbunga kibaya sana cha Katrina sasa kuna hatari ya kutokea kimbunga kingine ambacho ni hatari zaidi katika pwani ya Marekani. Kwa mujibu wa Maafisa wa Marekani, kimbunga hicho kinachoitwa Rita huenda kikapata nguvu zaidi kutokana na maji ya moto yaliyoko katika pwani ya Marekani. Kimbunga Rita kinaweza kusababisha madhara makubwa Florida, New Orleans na Texas. Mstahiki Meya wa New Orleans, Ray Nagin, ametoa mwito wa hatua kuchukuliwa mapema dhidi ya Rita. Amesema kuwa baadhi ya wakazi wa New Orleans, ambao wameanza kurejea baada ya kimbunga Katrina, wanalazimika kuondoka tena mjini humo. Mabwawa yaliyofanyiwa ukarabati hayataweza kukizuia hata kidogo kimbunga Rita. Bei ya mafuta ya petroli imeanza kupanda kwa asili mia saba mjini New York kutokana na kitisho cha kimbunga hicho.