Kimmel: Sakata langu limeweka mstari wa uhuru wa maoni
9 Oktoba 2025
Mchekeshaji maarufu wa Marekani Jimmy Kimmel amesema anatumai hasira ya umma kufuatia kusimamishwa kwa kipindi chake cha televisheni baada ya shinikizo kutoka kwa serikali ya Rais Donald Trump imeweka "mstari mwekundu” wa kulinda uhuru wa maoni nchini humo.
Kimmel aliondolewa hewani kwa muda mfupi mwezi uliopita baada ya kutoa maoni kufuatia mauaji ya mwanaharakati wa mrengo wa kulia Charlie Kirk, hatua iliyosababisha ghadhabu kubwa ya wananchi. Baada ya wiki moja, kituo cha ABC kinachomilikiwa na Disney kilirudisha kipindi chake hewani.
"Natumai tumepiga mstari mwekundu mkubwa sana kama Wamarekani kuhusu kile tunachokubali na kile tusichokubali,” alisema Kimmel.
Shinikizo kutoka Ikulu na FCC
Rais Trump amekuwa akikosoa sana utani anaofanyiwa na Kimmel na watangazaji wengine wa usiku, akiwaita "wahalifu wa maoni,” na mara kadhaa amedai vipindi vyao viondolewe hewani.
Kusimamishwa kwa Kimmel kulitokea muda mfupi baada ya mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya Shirikisho (FCC), Brendan Carr, kuashiria kwamba leseni za vituo vinavyorusha kipindi hicho zingechunguzwa iwapo havingekitekeleza agizo hilo.
Kimmel alisema maneno yake kuhusu muuaji anayedaiwa wa Kirk yalitafsiriwa vibaya "kwa makusudi na kwa nia ovu” na wanasiasa wa Republican.
Hata hivyo, alitania kuwa, "ningependa kumwalika Trump kwenye show yangu, lakini si lazima Carr.”
Kimmel alidhani imekwisha
Akizungumza katika mkutano wa Bloomberg Screentime mjini Los Angeles, Kimmel alikiri kwamba alidhani kipindi chake kingesitishwa kabisa baada ya kampuni kadhaa zinazomiliki zaidi ya vituo 40 tanzu vya ABC kuamua kususia matangazo yake.
"Nilimwambia mke wangu, ‘basi, ndiyo mwisho,'” alisema kwa utani.
Lakini kurejea kwake hewani kuligeuka kuwa hit kubwa ya watazamaji, licha ya kuwa robo ya taifa haikuweza kutazama kipindi hicho kutokana na ususiaji huo.
Chanzo: AFP