Kimpa Vita: Kiongozi wa Ukristo wa Kiafrika
3 Machi 2021Kimpa Vita aliishi kipindi gani?
Kimpa Vita alizaliwa mnamo mwaka1684 eneo la Mlima Kibangu katika ufalme wa Kongo, eneo ambalo leo hii ni sehemu ya Angola. Kimpa Vita anasemekana aligeukia maisha ya kiroho baada ya ndoa zake mbili kuishia kwenye talaka. Lakini pia inaripotiwa kuwa alikuwa na maono ya kimiujiza tangu umri mdogo.
Elimu ya Kimpa Vita ilikuwa ni ya aina gani?
Alizaliwa katika familia mashuhuri, na alipewa mafunzo kama nganga marinda, mganga mwenye uwezo wa kuwasiliana na wafu.
Kampa Vita anafahamika kwa lipi?
Katika kipindi kifupi cha maisha yake, alijulikana kwa uwezo wake wa kuunganisha Ufalme wa Kongo. Pia anakumbukwa kama mwanzilishi wa vuguvugu la Antonianist.
Vuguvugu hilo la Kimpa Vita lilikuwa linahusu nini?
Vuguvugu hilo la Antonianism linachanganya mafundisho ya dini na tamaduni tofauti: Kimpa Vita alichanganya mafundisho ya Ukristo pamoja na ya dini za jadi za Kiafrika. Mwishoni mwa maisha yake, alijitangaza kuzaliwa tena mara ya pili kama mtakatifu Anthony wa Padua, na kudai kwamba Yesu alikuwa mtu mweusi na alizaliwa Kongo. Miaka ya baadae kulizuka makundi mengine yanayochanganya dini ya Ukristo na mafundisho asilia ya Kiafrika kama vile Quimbanda naTocoismo.
Kimpa Vita alikufa vipi?
Mnamo mwaka 1706, alichomwa moto baada ya kutuhumiwa kwa kufanya uzushi wa kidini. Amri hiyo ya kuchomwa moto ilitolewa na Wakapuchini ambao ni watawa Wafransisko wa Kanisa Katoliki wakiongozwa na Friar Bernardo da Gallo.
Je, ni utata gani unaomzunguka Kimpa Vita?
Alipewa ujauzito na mmoja wa washirika wake. Wanajeshi wa Mfalme Pedro walimkamata wakati akiwa mafichoni, akimlea mtoto wake mchanga. Hadi hii leo, mtoto huyo haijulikani aliishia wapi. Mengi yanayojulikana kuhusu Kimpa Vita yanatokana na rekodi zilizowekwa na Friar Bernardo da Gallo, mtawa wa Wakapuchini aliyemhukumu kifo kwa kuchomwa moto. Kulingana na watawa hao, mtoto wa Kimpa Vita hakuuliwa. Hata hivyo simulizi za mdomo zinadai kuwa mtoto huyo mchanga alichomwa moto pamoja na mama yake mnamo mwaka 1706.
Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.