Kina cha maji cha ziwa Viktoria chashuka
14 Agosti 2007Watu Millioni 30 wanakaa pembezoni mwa ziwa hilo na kutegemea maji yake, samaki na aina nyingine ya matumizi. Lakini wakati huo huo, ziwa Viktoria linakabiliwa na matatizo mengi. Idadi ya aina ya samaki imapungua sana na pia kina cha maji kimeshuka.
Maji yanakwisha – hayo ndiyo maneno ya wimbo mmoja maarufu wa Kiluo unaojulikana sana mjini Kisumu. Kweli ni jambo linalotia wasiwasi vile kina cha maji kilivyoshuka haraka: Katika muda wa miaka 40 kimeshuka kwa mita mbili. Kama mtu ametoa plagi katika bafu.
Mwanasayansi wa mambo ya maji, Daniel Kull, anachunguza chanzo cha maendeleo haya. Naye anaeleza: “Nimeangalia vina vya maji vya ziwa la Viktoria katika miaka mitano au sita iliyopita na nimegundua kuwa kushuka kwa kina cha maji kunasababishwa na ukame kwa upande mmoja na sababu nyingine ni kwamba maji mengi mno yanatolewa na kutumika katika mabwawa.”
Miaka 50 iliyopita, Uganda imejenga bwawa la kwanza na imeanza kutumia ziwa la Viktoria kama kituo kikubwa cha umeme. Mwaka 2002 imejenga bwawa jingine na kituo kingine cha umeme. Tangu wakati huo, kina cha maji kinazidi kupungua. Hata serikali ya Uganda inapanga kujenga bwawa jingine.
Mtaalamu Daniel Kull anasema anashindwa kufikisha maonyo yake kwenye serikali hiyo: “Serikali na wizara za Uganda zinakataa kuzungumzia jambo hili. Wanakanusha kwamba kuna uhusiano kati ya mabwana na kushuka kwa kina cha maji.”
Karibu na Kisumu, wavuvi wamepanda boti zao. Wakaazi wengi wa eneo hili wanategemea uvuvi. Lakini tangu kina cha maji kupungua, idadi ya samaki wanazozivua imepungua. Shirika la “Rafiki wa ziwa Viktoria” linapigania kuhifadhi mazingira ya ziwa hilo. Huyu hapa Righa Makonge, msemaji mmoja wa shirika hilo: “Kenya inamiliki sehemu ndogo tu ya ziwa hilo, lakini samaki wanatumia sehemu hiyo kutagia mayai yao. Kutokana na kina cha maji kushuka, samaki hawawezi tena kufika maeneo haya ya kutaga mayai. Iwapo hali hii haitabadilika, ziwa Viktoria halitakuwa na samaki tena baada ya miaka michache.”
Wavuvi wengi tayari wanashindwa kulisha familia zao. Sababu nyingine ni kwamba aina ya samaki wadogo wanaliwa na sangara ambao wanauzwa pia nje. Hata wavuvi wazee wanasema hali imebadilika, kama anavyoeleza huyu hapa: “Ukilinganisha na zamani kuna tofauti kubwa. Zamani hii ilikuwa kazi nzuri, walikuwepo wavuvi wachache na samaki wengi. Hatukuenda mbali kuvua samani. Lakini leo inabidi tutumie nguvu zetu zote kufika maeneo ya mbali ambapo samaki wanapatikana na tunatumia nusu usiku.”
Zamani kabisa, kama miaka 14.700 iliyopita, ziwa la Viktoria lilikauka. Sasa hatari hii iko tena. Katika nyimbo zao watu wa Kisumu wanaomba maji yasiondoke.