1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinachoendelea kuhusu kuuawa mwandishi Jamal Khashoggi

22 Oktoba 2018

Uturuki leo imeimarisha uchunguzi wake kuhusu kifo cha mwandishi wa habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi. Wakati huohuo nchi za magharibi zimeongeza shinikizo dhidi ya Ufalme wa Saudi Arabia.

Türkei Recep Tayyip Erdogan, Präsident
Picha: Reuters/B. Szabo

Shirika la habari la serikali Anadolu limeripoti kwamba waendesha mashitaka kadhaa wa Uturuki waliwahoji mashahidi watano ambao ni wafanyakazi wa ubalozi huo mdogo kuhusiana na kifo cha Khashoggi. Kwa mujibu wa shirika la habari la NTV la nchini Uturuki, gari la balozi mdogo wa Saudi Arabia limepatikana katika mji wa Sultangazi ulio katika wilaya ya Istanbul. Na taarifa zinasema kuwa polisi watalichunguza gari hilo.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameapa kufichua ukweli wote kuhusu mauaji ya mwandishi huyo wa habari Jamal Khashoggi  akisisitiza  kwamba kwamba nchi yake ina wajibu wa kuueleza ulimwengu ukweli kuhusu kilichotokea. Erdogan anatarajiwa kutoa taarifa kamili kesho kuhusu kifo cha Khashoggi.

Saudi Arabia  ilikiri mwishoni mwa wiki  kuwa Khashoggi aliuawa katika ubalozi wake mdogo ulioko Istanbul, lakini imesema haijui ulipo mwili wake na mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Mohamed bin Salman amesisitiza kuwa hakufahamu juu ya operesheni ya kumuua mwandishi huyo aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wake.

Mwandishi wa habari aliyeuawa Jamal KhashoggiPicha: picture-alliance/AA/O. Shagaleh

Ujerumani imezisisitizia nchi za Umoja wa Ulaya kuonyesha ushirikiano katika suala la mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliwaambia waandishi wa habari mjini Berlin kwamba anaunga mkono hatua ya kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia kufuatia mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi.

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Peter Altmaier, anayehusika na kuidhinisha mauzo ya silaha, aliiambia televisheni ya Ujerumani ya ZDF kwamba kwa wakati huu, hawezi kuidhinisha mauzo yoyote ya silaha kabla ya kubainika kilichotokea.

Wakati huo huo wafanya biashara wakuu na wawakilishi wa Ulaya wamejitenga na Saudi Arabia tangu sakata la kutoweka na kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, na wengi wamesema hawatahudhuria mkutano wa uwekezaji wa wiki hii. Falme hiyo ya Kiarabu ilikuwa na matumaini kwamba mkutano huo ungelitumika kujijenga na kuongeza umaarufu wake kimataifa.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/AP/AFPE/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW