1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinjeketile Ngwale - kiongozi wa vita vya Maji Maji

2 Januari 2018

Kinjeketile Ngwale anachukuliwa kama ishara ya upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani huko Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania. Alidai kwamba yeye ni roho na angeweza kuwalinda Watanganyika dhidi ya Wakoloni.

Aliishi: Ngarambe, Matumbi huko Tanganyika ambayo kwa sasa ndiyo Tanzania. Alinyongwa mwezi Agosti mwaka 1905 na maafisa wa Ujerumani kwa kosa la uchochezi.

Anafahamika sana kwa: kupagawa na Hongo ambaye ni roho. Kulingana na mkongwe huyo, roho huyo alijitokeza kama nyoka, akamburuza Kinjeketile chini ya maji na alipoibuka baada ya saa ishirini na nne, alikuwa amekauka na akaanza kufanya utabiri.

Anafahamika pia kwa kuyaunganisha makabila ya eneo hilo na maeneo mengineneyo kadri ujumbe wake ulivyozidi kusambaa, na kuweza kuwa mtu wa kwanza kuleta utaifa Tanganyika.

Anajulikana pia kwa kuwaambia wafuasi wake kwamba iwapo watatumia maji yake yaliyo na dawa, risasi za Wajerumani hazingewaingia.

Anafahamika kwa kuwa mwanzilishi wa vita vya Maji Maji, ingawa yeye mwenyewe alikufa muda mfupi baada ya vuguvugu hilo kuanza. Vita vya Maji Maji vilianza mwaka 1905 na kuisha 1907 na vilikuwa mojawapo ya vita vikuu dhidi ya ukoloni barani Afrika.

Alikashifiwa kwa: kuchangia kwa vifo vya watu wengi baada ya kuwadanganya kwamba maji yangewakinga dhidi ya risasi. Inakadiriwa kwamba kati ya watu 180,000 na 300,000 walifariki dunia wakati wa vita vya Maji Maji kutokana na mapigano na njaa, jambo lililopunguza idadi ya watu kwa thuluthi moja.

Mwaka wa 1969 mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Tanzania Ebrahim Hussein alichapisha mchezo wake "Kinjeketile" kuhusu maisha ya mwasisi huyo na vita vya Maji Maji.

Mwandishi: Jacob Safari

Mhariri: Gakuba Daniel 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW