Kinshasa. DRC kupatiwa msaada na benki kuu ya dunia.
10 Machi 2007Rais wa benki ya dunia Paul Wolfowirtz akiwa katika ziara ya siku mbili kuitembelea jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, jana amesema kuwa nchi hiyo ya Afrika ya kati itapatiwa kiasi cha dola bilioni 1.4 kama msaada katika muda wa miaka mitatu ijayo.
Nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini inarejea katika hali ya kawaida baada ya kuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1998-2003 ambavyo vimesababisha mamilioni ya watu kupoteza maisha , wengi wao kutokana na matatizo yaliyosababishwa na vita hasa ukosefu wa chakula na magonjwa.
Uchaguzi wa mwaka jana ulisifiwa kuwa ni uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia katika muda wa miongo mine.
Wolfowitz amesema kuwa msaada huo wa kwanza wa benki hiyo chini ya utaratibu uliorahisishwa kwa mataifa ambayo yanamahitaji ya haraka utakuwa ni dola milioni 180 ili kujenga upya miundo mbinu katika mji mkuu Kinshasa ambayo imeharibika.