Kinshasa. Watu wanane wauwawa katika kampeni.
29 Julai 2006Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo , DRC , inajiweka tayari leo kwa ajili ya uchaguzi wa vyama vingi katika historia yake ya miaka 46 baada ya kutokea umwagaji wa damu kabla ya uchaguzi huo hapo kesho ambapo watu wanane wameuwawa katika machafuko yanayohusiana na kampeni za uchaguzi.
Polisi mmoja ambaye alikuwa anamlinda mgombea wa kiti cha urais Azarius Ruberwa alipigwa risasi na kufa jana Ijumaa usiku wakati polisi hao waliporushiana risasi na walinzi wa rais Joseph Kabila nje kidogo ya mji wa Kinshasa.
Msemaji wa umoja wa mataifa amesema kuwa watu wengine wawili wamejeruhiwa katika mapigano hayo ambayo yametokea wakati Kabila , mgombea anayeonekana kuwa anaweza kupata ushindi katika uchaguzi huo, alikuwa anaelekea katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni kabla ya kampeni kumalizika usiku wa manane.
Wakati huo huo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan ametoa wito wa utulivu katika nchi hiyo wakati inakaribia kufanya uchaguzi huo wa kihistoria. Kiongozi huyo wa umoja wa mataifa amewataka Wakongo kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kujiepusha na ghasia.
Kiasi cha wanajeshi 19,000 wa umoja wa mataifa na umoja wa Ulaya wako nchini humo kusaidia kuhakikisha uchaguzi wa kesho unafanyika kwa usalama.