1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinyang'anyiro cha Bundesliga chashika kasi

1 Februari 2021

Bayern Munich bado wapo kileleni mwa Bundesliga baada ya jumla ya mechi 19 kuchezwa wakiwa wana pointi 45 na haya yote ni baada ya kuvuna ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya TSG Hoffenheim katika uwanja wa Allianz Arena.

Bundesliga - Bayern Munich v TSG 1899 Hoffenheim
Picha: Andreas Gebert/REUTERS

Kipigo hiki walichowapa Hoffenheim kilikuwa ni kama wanalipiza kisasi kwani katika mechi ya kwanza baina yao msimu huu Hoffenheim ndio walioebuka kidedea.

Hansi Flick ni mkufunzi wa Bayern Munich

"Ushindi wa 4-1 kwetu sisi ni ushindi mkubwa lakini si eti kila kitu kilikuwa sawa kwa asilimia 100, lakini umeniridhisha kwa kweli. Hii ni mechi ya nne mfululizo ambayo tumeishinda kwa hiyo ni matokeo mazuri," alisema Flick.

Ni ushindi muhimu kwa Leipzig baada ya kufungwa na Mainz

Katika nafasi ya pili Bayern wanafuatwa na RB Leipzig ambao pointi walizo nazo ni 38 na wamefika hapo baada ya kuwazidi kete Bayer Leverkusen moja bila jawabu kwenye mechi yao waliyoicheza uwanjani Red Bull Arena mwishoni mwa wiki ambapo Christopher Nkunku ndiye aliyekuwa mfungaji wa goli hilo la pekee.

Wachezaji wa Leipzig wakisherehekea goli dhidi ya Bayer LeverkusenPicha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Baada ya kuulizwa umuhimu wa ushindi huu, kiungo wa RB Leipzig, Kevin Kampl, alikuwa na haya ya kusema.

"Ni ushindi muhimu sana. Sisi wenyewe kama wachezaji tulisemezana baina yetu kwamba ni muhimu sana kupata ushindi leo hasa baada ya kushindwa na Mainz mwishoni mwa wiki iliyopita. Na ni fahari kubwa kwetu sote kwasababu ni ushindi tulioupata dhidi ya timu mahiri. Tunafahamu kwamba tunastahili kuendelea vivyo hivyo," alisema Kampl.

Wolfsburg wanaimiliki nafasi ya tatu kwenye jedwali wakiwa na pointi 35 baada ya kuwashinda Freiburg 3-0 hapo jana hii ikiwa ni ishara ya mchezo mzuri wanaouonyesha Wolfsburg tangu kuanza kwa msimu huu. Eintrach Frankfurt wamepanda jedwali hadi katika nafasi ya nne pointi zao zikiwa 33 baada ya ule ushindi wa 3-1 walioupata wakicheza na Hertha Berlin kisha tano bora inafungwa na Bayer Leverkusen walio pointi moja nyuma ya Frankfurt.

Unaposhinda mechi ni vizuri kufurahia

RB Leipzig kileleni mwa ligi ya Bundesliga

This browser does not support the audio element.

Borussia Dortmund wana pointi sawa na Leverkusen 32, ila wamedunishwa na uchache wa mabao ndio sababu wanaishikilia nafasi ya sita licha ya kushinda mchuano wao uliopita 3-1 walipokuwa uwanjani kucheza na Augsburg.

Kocha wa Dortmund Edin TerzicPicha: imago images/Picture Point LE

Kocha wa Dortmund Edin Terzic anaizungumzia mechi hiyo.

"Mpira ndio mchezo mzuri kabisa duniani kote na la muhimu ni kushinda mechi. Kwa hiyo unapokuwa katika kiwango kizuri cha mchezo kama hiki na upate ushindi kama huu, unastahili kufurahia na ndivyo tulivyofanya. Sijaitazama mechi hii kwenye televisheni tena ila nimeifurahia sana," alisema Terzic.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW