1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Malta Joseph Muscat kujiuzulu.

2 Desemba 2019

Waziri mkuu wa Malta Joseph Muscat ameliambia taifa hilo jana usiku kwamba atajiuzulu mwezi Januari kufuatia shinikizo kutoka kwa wananchi walio na ghadhabu kutokana na ukweli kuhusu mauaji ya mwanahabari.

Malta Premierminister Joseph Muscat
Picha: picture-alliance/AP Photo

Katika taarifa kupitia runinga, Muscat amesema amemuarifu rais wa nchi hiyo kwamba atajiuzulu kama kiongozi wa chama cha Labour kinachoongoza tarehe 12 mwezi Januari mwakani na kwamba katika siku zijazo, atajiuzulu kama waziri mkuu. Muscat aliongeza kusema kuwa taifa hilo halifafanuliwi kutokana na watu binafsi na kwamba ni kuu kuliko yeye. Amesema kuwa atamwandikia rais wa chama cha Labour ili mchakato wa kumchagua kiongozi mpya wa chama hicho uanze tarehe 12 mwezi Januari, 2020. 

Saa chache kabla ya hayo takriban raia elfu 20 wa nchi hiyo walifanya maandamano nje ya mahakama moja katika mji mkuu wa nchi hiyo, Valletta, wakimtaka ajiuzulu hii ikiwa idadi kubwa zaidi ya waandamanaji kujitokeza katika maandamano ya kila siku katika wiki za hivi karibuni. Akianza hotuba yake, Muscat alisema kuwa kama waziri mkuu, aliahidi miaka miwili iliyopita kwamba haki itatekelezwa katika kisa cha mauaji ya Daphne Caruana Galizia na kwamba ametimiza ahadi yake. Lakini familia ya mwandishi huyo wa habari aliyeuawa imesema kuwa Muscat anapaswa kujiuzulu sasa na kutishia maandamano zaidi iwapo hatajiuzulu mara moja.

Waandamanaji wabeba mabango katika maandamano ya kutaka haki ya mauaji ya mwanahabari.Picha: Reuters/Y. Nardi

Katika taarifa jana usiku, familia hiyo ilisema kuwa, ''Kuendelea kuhudumu kwake kama waziri mkuu hakuvumiliki kwa yeyote anayejali kuhusu haki. Jukumu lake katika uchunguzi wa mauaji ya mke wetu na mama yetu ni kinyume cha sheria.''Mwana wa kiume wa mwanahabari huyo aliyeuawa, Matthew Caruana Galizia ambaye pia ni mwandishi habari, aliandika katika ukurasa wake wa twitter, ''watu watajitokeza barabarani tena hapo kesho.'' Muscat amekuwa akikabiliwa na shinikizo kali za kujiuzulu huku watu walio karibu naye serikalini wakihusishwa na uchunguzi wa mauaji ya Caruana Galizia aliyeuawa katika mlipuko wa bomu mwaka 2017.

Mwanahabri huyo aliyekuwa akiripoti kuhusu ufisadi alikuwa amefichua ufisadi unaofanywa na serikali katika habari zake.Mapema wiki hii mawaziri wawili na Keith Schembri ambaye ni katibu mkuu kiongozi wa Muscat, waliachia ngazi baada ya kuhusishwa na uchunguzi huo. Schembri alikamatwa siku ya Jumanne na kuachiliwa bila ya mashtaka siku ya Alhamisi.

Waziri huyo mkuu amekuwa akitarajiwa kujiuzulu tangu siku ya Jumapili asubuhi baada ya kuitishwa kwa mkutano wa dharura wa chama chake cha Labour. Hii ni kulingana na mbunge mmoja mwenye cheo aliyeliambia shirika la habari la dpa mapema jana .Hata hivyo katika taarifa yake Muscat hakutaja matakwa ya umma ya kumtaka ajiuzulu mara moja na kusema kuwa yeye sio mkamilifu na kwamba ana makosa yake pia. Tangazo la Muscat pia lilikosolewa vikali na wabunge wanaoamini kuwa afisi hiyo imeharibiwa sifa kwa sababu ya kuhusishwa na mauaji hayo.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wa Twitter, kiongozi wa upinzani Adrian Delia amesema kuwa kuchelewa kujiuzulu kwa Muscat ni pigo kwa haki na kusisitiza kuwa anapaswa kuondoka mara moja.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW