1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi mkuu wa upinzani Congo Etienne Tshisekedi afariki

1 Februari 2017

Kiongozi mkuu wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Etienne Tshisekedi, ameaga dunia Jumatano (01.02.2017) mjini Brussels, Ubelgiji, akiwa na umri wa miaka 84.

Demokratische Republik Kongo Etienne Tshisekedi gestorben
Picha: Reuters/F. O'Reilly

Tshisekedi alikuwa mshirika mkubwa wa kiongozi wa zamani wa Congo, Mobutu Sese Seko, aliyeitawala nchini kwa miongo kadhaa, zamani ikijulikana kama Zaire, kabla kupinduliwa na Rwanda, Uganda na vikosi vingine. Baadaye lakini Tshisekedi aligeuka na kuwa mpinzani mkubwa wa Mobutu. Alikuwa pia mpinzani mashuhuri wa rais Laurent Kabila, aliyetwaa madaraka mnamo mwaka 1997, na mtoto wake rais wa sasa Joseph Kabila, ambaye ameiongoza Congo tangu mwaka 2001.

Tshisekedi, kiongozi ambaye hakuonekana sana hadharani kwa kipindi kirefu katika miaka ya hivi karibuni kutokana na afya yake iliyozorota, alikuwa amesafiri kutoka Kinshasa kwenda Brussels siku ya Jumanne, wakati ambapo Congo iko katika wakati muhimu sana kisiasa.

Muungano wa upinzani aliokuwa akiuongoza unafanya mashauriano juu ya hatua za kuchukuliwa katika mkataba wa kugawana madaraka uliosainiwa mkesha wa mwaka mpya kuepusha machafuko mapya baada ya rais Kabila kukataa kuondoka madarakani muhula wake ulipokamilika mwezi Desemba mwaka uliopita.

Maaskofu wa kanisa Katoliki, CongoPicha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Mkataba huo uliosimamiwa na maaskofu wenye ushawishi mkubwa wa kanisa Katoliki nchini humo unamruhusu rais Kabila kubakia madarakani hadi mwisho wa mwaka huu sambamba na serikali ya mpito na waziri mkuu mpya ambaye wajumbe wa serikali na upinzani bado hawajakubaliana.

Hali ya Mzee ilikuwa mbaya

Kabla kifo chake, chama cha Tshisekedi, Muungano kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii (UPDS) kilisema angerejea Congo kuendelea na majukumu yake ya kihistoria, lakini kulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya "Mzee" kama alivyokuwa akijulikana kote nchini.

Baada ya miaka miwili ya matibabu katika mkoloni wa zamani wa Congo, Ubelgiji, Tshisekedi alirejea kwa shangwe na nderemo mwezi Julai mwaka uliopita huku mamia ya maelfu ya watu wakijitokeza barabarani kumkaribisha nyumbani.

Historia fupi ya Tshisekedi

Tshisekedi akijulikana pia kwa jina la utani "Sphinx of Limete" -- kitongoji cha mji wa Kinshasa alikoishi. Alizaliwa Desemba 14, 1932 jimboni Kasai Occidental --mji wa nyumbani Kananga uliitwa Luluabourg katika ile iliyojulikana kama Congo ya Ubelgiji. Tshisekedi alipata shahada ya kwanza ya uzamivu katika masomo ya sheria ya Congo iliyokuwa imepata huru akiwa na umri wa miaka 29. 

Alikuwa bado mwanafunzi wakati kanali kijana wa jeshi, Joseph Desire Mobutu, alipotwaa madaraka na kutangaza alikuwa amempindua waziri mkuu maarufu wa zamani, Patrice Lumumba na rais Joseph Kasa-Vubu. Tshisekedi aliteuliwa katika jopo la makamishna ambao Mobutu aliwateua kuendesha serikali, ambayo Januari 1961 ilisaini waranti wa kukamatwa Lumumba. Lumumba aliuawa baada ya kutiwa ndani.

Baada ya Mobutu kufanya mapinduzi Novemba 1965, Tshisekedi alihudumu kama waziri wa mambo ya ndani, sheria na mipango ya taifa, na alikuwa katibu wa kwanza wa chama cha Mobutu.
Alichaguliwa tena mbunge 1970, lakini baadaye akatofautiana na Mobutu, wakati yeye na wabunge wengine 12 walipoandika barua ya wazi kupinga utawala wa kifisadi na maonevu wa dikteta huyo. Alitupwa gerezani na kuachiwa huru 1982, mwaka aliokiasisi chama cha UDPS, kilichokuja kuwa chama kikuu cha upinzani baada ya Mobutu kuondosha marufuku dhidi ya vyama vya siasa 1990.

Rais Joseph KabilaPicha: picture alliance/AP Images/J. Bompengo

Akipigania mageuzi ya demokrasia kuondokana na utawala wa Mobutu, Tshisekedi alichaguliwa kuwa waziri mkuu Agosti 1992, lakini Mobutu akamtimua siku tatu baadaye. Tshisekedi hata hivyo aliendelea kushikilia nafasi hiyo kwa miezi saba, ingawa serikali aliyoiongoza haikutambuliwa na Mobutu.

Baada ya Mobutu kupinduliwa 1997 katika mapinduzi yaliyoongozwa na Laurent Desire Kabila, babake rais wa sasa, Joseph Kabila, Tshisekedi kwa haraka aligeuka kuwa mpinzani wa utawala mpya -- msimamo ambao uliendelea baada ya Laurent Kabila kuuliwa 2001 na baadaye mtoto wake, Joseph Kabila, kuingia madarakani.

Tshisekedi alipenda amani

Tshisekedi alisaini mkataba wa amani uliovifikisha mwisho vita vya kati ya 1998 - 2003 vilivyozuka baada ya Mobutu kupinduliwa, lakini alikataa kushiriki katika serikali ya mpito ya Laurent Kabila.

Tshisekedi aliususia uchaguzi wa 2006, uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kuwahi kufanyika Congo katika kipindi cha zaidi ya miaka 40, kutokana na madai ya wizi wa kura. Mwaka 2007 alisafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Alirejea Congo 2010 kushindana na rais Kabila katika uchaguzi wa urais, na aliposhindwa katika uchaguzi huo wa Novemba 2011 uliogubikwa na utata, Tshisekedi alijitangaza mwenyewe kuwa ndiye rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Akiwa na shauku la kuepusha machafuko katika nchi inayokabiliwa na mgogoro, Tshisekedi alisaidia kuuleta pamoja upinzani katika muungano ambao mwaka uliopita, ingawa kwa shingo upande, ulikubali kumruhusu rais Kabila abakie madarakani kwa muda.

Felix TshisekediPicha: Reuters/K. Katombe

Mmoja kati ya watoto watano wa Tshisekedi, Felix, ana matumaini ya kutangazwa waziri mkuu katika serikali ya mpito inayojiandaa kuiongoza Congo, taifa lenye utajiri mkubwa wa madini lenye ukubwa unaokaribiana na Ulaya Magharibi.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/reuters/dpae

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW